Mjumbe wa UN apongeza misimamo ya Hamas kuhusu uchaguzi
Mratibu Maalumu wa Amani wa Umoja wa Mataifa katika kanda ya Mashariki ya Kati amepongeza misimamo ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) kuhusu suala la kuitishwa uchaguzi mkuu huko Palestina.
Nikolay Mladenov amesema katika mazungumzo yake na viongozi wa Hamas huko katika Ukanda wa Gaza kwamba, makubaliano ya kitaifa ya Wapalestina kwa ajili ya kuitishwa uchaguzi ni jambo la dharura.
Mratibu wa Masuala ya Kkibinadamu wa Umoja wa Mataifa katika Kanda ya Mashariki ya Kati Nikolay Mladenov aliwasili jana katika Ukanda wa Gaza.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Siasa ya Hamas, Ismail Haniya ametilia mkazo msimamo chanya wa harakati hiyo kuhusu suala la kuitishwa uchaguzi katika ardhi za Palestina na kusema: Makundi mengine ya Kipalestina pia yamekaribisha suala hilo.
Uchaguzi wa mwisho ulifanyika mwaka 2006 huko Palestina. Katika uchaguzi huo Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) iliibuka na ushindi. Tangu wakati huo yaani miaka 13 iliyopita, hakujafanyika uchaguzi wa aina yoyote huko Palestina na makundi mbalimbali yanakosoa suala hilo yakiitaka Mamlaka ya Ndani kuitisha uchaguzi mkuu.