Yemen: Saudia inafanya juhudi za kuanzisha mawasiliano na Answarullah
Mshauri wa Baraza Kuu la Kisiasa nchini Yemen anayehusika na masuala ya kidiplomasia ameelezea juhudi zinazofanywa na Saudia kwa ajili ya kuanzisha uhusiano na harakati ya wananchi ya Answarullah ya nchi hiyo.
Abdul-Ilah Hajar, ameyasema hayo katika mahojiano na kanali ya televisheni ya al-Mayadin na kuongeza kuwa, tangu awali Saudia ilikuwa ikifanya juhudi kupitia balozi wake na baadhi ya Wayemen kujaribu kuanzisha uhusiano na harakati hiyo na kwamba hivi sasa Riyadh imezidisha juhudi hizo. Akisisitiza suala la kuhitimishwa vita nchini humo amesema kuwa, hatua yoyote ya kurejesha amani, inapasa kutilia maanani masharti ya Yemen la sivyo, iwapo juhudi za amani zitakumbwa na ukwamishaji mambo wa muungano vamizi wa Saudia, basi muqawama wa Wayemen utaendelea.
Jumatano iliyopita afisa mmoja wa Saudia alikiri kwamba nchi yake inafanya mazungumzo na Sana'a kwa ajili ya kuhitimisha vita nchini Yemen. Itakumbukwa kuwa Saudia kwa uungaji mkono wa Marekani, Imarati na baadhi ya nchi nyingine ilianzisha mashambulizi makali dhidi ya Yemen mwezi Machi 2015, sambamba na kuizingira nchi hiyo ya Kiarabu katika pande tatu za ardhini, angani na baharini. Hadi sasa vita hivyo vimepelekea zaidi ya watu elfu 16 kuuawa na makumi ya maelfu ya wengine kujeruhiwa. Aidha hadi sasa mamilioni ya Wayemen wamekuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi hiyo.