Harakati ya Hizbullah ya Lebanon yasisitiza kutetewa Palestina
Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon amesisitiza udharura wa kuungwa mkono na kutetewa taifa madhulumu la Palestina.
Sheikh Naim Qassim amesema hayo hapa mjini Tehran pambizoni mwa Mkutano wa 33 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu ambapo sambamba na kuashiria maudhui ya mkutano huo amesisitiza umuhimu wa kutetewa Msikiti Mtakatifu wa al-Aqswa na Palestina kwa ujumla.
Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amebainisha kuwa, kufanyika Mkutano wa Umoja wa Kiislamu katikka kipindi hiki ni kusisitiza kwamba, lengo la mhimili wa muqawama katika eneo hili ni moja.
Kadhalika amesisitiza kuwa, Quds haiwezi kugawanywa katika maeneo mawili ya mashariki na magharibi kwani haiwezekani kuigawa ardhi ya taifa fulani.
Katibu Mkuu wa Hizbullah amesisitiza pia kuwa, utawala haramu wa Israel umeshindwa katika vita vyake vya ana kama ambavyo imepoteza pia mamluki wake wengi na wenzo wa utakfiri katika nchi mbalimbali.
Kiongozi huyo wa ngazi za juu wa Hizbullah amesema pia kuwa, tunawatangazia walimwengu kwamba, Iran ndio mhimili na kamanda wa muqawama na mapambano.
Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon amesema bayana kwamba, ubeberu wa Kimarekani ni kinara na kiongozi wa dhulma, udikteta na jinai mbalimbali katika maeneo tofauti ulimwenguni.