Walowezi wa Kizayuni wavamia tena Msikiti Mtakatifu wa al-Aqswa
(last modified Wed, 18 Dec 2019 11:41:39 GMT )
Dec 18, 2019 11:41 UTC
  • Walowezi wa Kizayuni wavamia tena Msikiti Mtakatifu wa al-Aqswa

Walowezi wa Kizayuni leo wameuvamia tena Msikiti wa al-Aqswa huko Palestina wakisaidiwa na askari wa jeshi la utawala haramu wa Israel na kuuvunjia heshima msikiti huo ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu.

Walowezi hao  wa Kizayuni baada ya kuingia katika eneo la ndani la msikiti huo mtakatifu walisikika wakipiga nara dhidi ya Uislamu na Waislamu.

Vyombo vya habari vya Palestina vimeripoti kwamba, hujuma na uvamizi huo umefanyika kwa msaada na uungaji mkono wa wanajeshi wa utawala ghasibu wa Israel.

Vitendo vya kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu vinafanyika katika hali ambayo, viongozi wa nchi za Kiarabu na jamii ya kimataifa wameendelea kunyamaza kimya na kutochukua hatua zozote za kukabiliana na vitendo hivyo.

Kwa mujibu wa duru za Kipalestina, karibu kila siku walowezi wa Kizayuni wamekuwa wakifanya uvamizi katika msikiti huo lengo likiwa ni kutekeleza njama za kutokomeza utambulisho wa Kiislamu na Kikristo wa Msikiti wa al-Aqswa na badala yake kuweka nembo za Kizayuni.

aqswa

Walowezi wa Kizayuni wakipiga nara dhidi ya Uislamu baada ya kuvamia Msikiti wa al-Aqswa

Katika miaka ya hivi karibuni, utawala wa Kizayuni wa Israel umeshadidisha hujuma na uvamizi wake dhidi ya maeneo ya Wapalestina ukifanya njama za kufikia malengo yake haramu katika ardhi za Wapalestina.

Hata hivyo kusimama kidete wananchi wa Palestina hadi sasa kumekwamisha njama na mipango yote ya Wazayuni, zikiwemo njama zake za kubadilisha muundo wa kijamii na kijiografia wa Baytul Muqaddas.

Uvamizi huo unakwenda sambamba na ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi ya Palestina.