Hamas: Kufanyika uchaguzi Quds hakuhitajii ruhusa ya Israel
(last modified Thu, 26 Dec 2019 01:11:14 GMT )
Dec 26, 2019 01:11 UTC
  • Hamas: Kufanyika uchaguzi Quds hakuhitajii ruhusa ya Israel

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imetangaza kuwa kufanyika uchaguzi katika mji wa Quds hakuhitajii ruhusa ya Israel na kwamba utawala huo wa Kizayuni unapasa kufahamishwa suala hilo.

Salah al Bardawil mwanachama wa ngazi ya juu wa harakati ya Hamas amesema kuwa hakuna uchaguzi utakaofanyika bila ya kuishirikisha Quds. Amesema kuwa Mahmoud Abbas Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina hapasi kuusubiri utawala wa Kizayuni utoe kibali ndipo naye atoe agizo la Rais katika uwanja huo. Al Bardawil aliyasema hayo jana Jumatano akijibu matamshi ya Mahmoud Abbas kuhusu uchaguzi huko Quds.  

Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Paestina 

Al Bardawil ameongeza kuwa uchaguzi huko Quds ni mstari mwekundu; na matamshi ya Mahmoud Abbas kwa ajili ya kupata ruhusa kutoka kwa utawala wa Kizayuni ili uchaguzi huo upate kufanyika ni mshtuko mkubwa kwa raia wote wa Palestina kwa sababu Quds ni mji mkuu na wa kudumu milele wa Palestina. 

Wakati huo huo Hamas imemuandikia barua  Hana Nasir Mkuu wa Kamati Kuu ya Uchaguzi ya Palestina ikisisitiza kuwa utawala wa Kizayuni hauna mamlaka ya kusitisha mchakato wa uchaguzi na kwamba haitasubiri ruhusa ya utawala huo ili kuendesha uchaguzi. 

Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina Jumanne wiki hii alisema kuwa makundi yote ya Palestina yameafiki kufanyika uchaguzi hata hivyo bado kuna kizuizi kikubwa yaani utawala wa Kizayuni ambao unapinga kufanyika uchaguzi huko Quds. 

 

Tags