Kuendelea utata kuhusu kufanyika uchaguzi wa Palestina
Baada ya kupita zaidi ya miezi mitatu tokea Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina (PA) atangaze azma ya kufanyika uchaguzi, bado kunaendelea kushuhudiwa utata na hitilafu kuhusu kadhia hiyo.
Mnamo Septemba 2019, katika mkutano wa kila mwaka wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Mahmoud Abbas alitangaza kuwa tayari kwa ajili ya uchaguzi wa bunge na rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina. Tangazo hilo la Abbas lilipokelewa vizuri na makundi ya Palestina hasa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas).
Uchaguzi wa kwanza wa Bunge la Palestina ulifanyika mwaka 1996 nao uchaguzi wa pili ukafanyika mwaka 2006 ambapo Hamas ilipata ushindi mkubwa. Hivi sasa baada ya kupita takribani miaka 14 hakuna ishara zozote za wazi za kufanyika uchaguzi wa tatu wa Bunge la Palestina.
Tatizo la kwanza linahusu namna ya kufanyika uchaguzi huo. Hamas inataka kufanyika uchaguzi mkuu Palestina ambao utajumuisha uchaguzi wa rais, bunge na mabaraza ya serikali za mitaa. Baadhi ya makundi ya Palestina yanasisitiza tu kuhusu kufanyika uchaguzi wa bunge.
Tatizo la pili ni kuhusu eneo la kijiografia la kufanyika uchaguzi huo. Harakati ya Hamas inasisitiza kuwa uchaguzi huo ni lazima ufanyike katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, Ukanda wa Ghaza na Quds (Jerusalem) inayokaliwa kwa mabavu na Israel. Hii ni katika hali ambayo Mamlaka ya Ndani ya Palestina inasema uchaguzi wa Quds ufanyike tu kwa idhini ya utawala haramu wa Israel. Hamas inasisitiza kuwa, Quds Mashariki ni ardhi ya Palestina kwa mujibu wa hali ya hivi sasa na kwa msingi huo hakuna haja ya kuomba idhini ya Israel ili kuandaa uchaguzi katika eneo hilo.
Kuhusiana na nukta hiyo, mwanacahama wa ngazi za juu wa Hamas, Salah al-Bardawil, amemtaka Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, atoe amri maalumu ya kufanyika uchaguzi mjini Quds bila ya kuomba ruhusa kutoka kwa utawala wa Kizayuni wa Israel.
Al-Bardawil ameongeza kuwa: "Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) inawatangazia Wapalestina na wasiokuwa Wapalestina pamoja na mataifa yote ya Kiislamu na Kiarabu kuwa, hakuna uchaguzi utakaofanyika bila kuwepo upigaji kura katika mji wa Quds."
Sera zinazofuatwa sasa na Mamlaka ya Ndani ya Palestina zimewahi kushuhudiwa huko nyuma. Mwaka 2012, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina alichukua uamuzi wa kuandaa uchaguzi wa serikali za mitaa katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan lakini hakuitisha uchaguzi huo katika Ukanda wa Ghaza. Uamuzi huo wa Abbas ulilalamikiwa vikali na Hamas ambayo iliususia uchaguzi huo. Kwa msingi huo iwapo Hamas itaamua kususia uchaguzi ujao wa Palestina basi utakuwa ni uchaguzi dhaifu, duni sana na utakaokumbwa na changamoto za uhalali.
Kwa kuzingatia hali hiyo, inaelekea kuwa, makundi ya Palestina hayako tayari kwa ajili ya uchaguzi. Hii ni katika hali ambayo katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, hasa baada ya kumalizika muda wa kuhudumu Serikali ya Maelewano ya Kitaifa na kuarifishwa waziri mkuu mpya Machi 2019, kumeongezeka hitilafu na migongano baina ya makundi ya Palestina.
Kufanyika uchaguzi kunaweza kupunguza hitilafu hizo na hivyo kuwafanya Wapalestina wapate umoja na hii ndiyo nukta ambayo pia imesisitizwa na Waziri Mkuu wa Palestina.
Waziri Mkuu wa Palestina, Mohammad Shtayyeh, ameashiria kuhusu umuhimu wa kuwepo umoja miongoni mwa mirengo ya Wapalestina na kuwa misimamo ya pamoja itapelekea kuhitimishwa changamoto za sasa na hitilafu zilizopo. Ni wazi kuwa umoja wa makundi ya Wapalestina utawawezesha kuelekeza nguvu zao katika mapambano yao ya kukabiliana na utawala dhalimu wa Israel.