Maaskofu wa Kikatoliki wataka kutambuliwa rasmi nchi huru ya Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i58614-maaskofu_wa_kikatoliki_wataka_kutambuliwa_rasmi_nchi_huru_ya_palestina
Maaskofu wa Ulaya, America ya Kaskazini na Afrika Kusini amezitaka nchi zao kuitambua rasmi nchi huru ya Palestina na kusisitiza udharura wa kuwapa Wapalestina haki zao zote.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 19, 2020 07:56 UTC
  • Maaskofu wa Kikatoliki wataka kutambuliwa rasmi nchi huru ya Palestina

Maaskofu wa Ulaya, America ya Kaskazini na Afrika Kusini amezitaka nchi zao kuitambua rasmi nchi huru ya Palestina na kusisitiza udharura wa kuwapa Wapalestina haki zao zote.

Maaskofu 34 wa Kanisa Katoliki wa kundi Holy Land Coordination walioko safarini katika miji wa Ramallah na Quds (Jerusalem) wametoa taarifa wakitangaza uungaji mkono wao kwa Wapalestina na kusema wamehamasishwa na uvumilivu wa kudumu wa watu waliokutana nao huko Gaza, Quds Mashariki na Ramallah licha ya hali zao mbaya.

Taarifa iliyotolewa na maaskofu hao imetilia mkazo udharura wa kuheshimiwa sheria za kimataifa na kutambuliwa rasmi nchi ya Palestina, haki ya watu wote kuishi kwa amani, upinzani wa sera za kuwalinda na kuwasaidia kiuchumi na kisiasa walowezi wanaoishi katika ardhi za Palestina zilizoghusubiwa na Israel na upinzani mkubwa dhidi ya ukatili na ukiukaji wa haki za binadamu unaofanyika katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na Israel.  

Maaskofu hao wa kikatoliki wamesema kuwa, hali ya maisha katika maeneo ya Palestina hususan katika Ukingo wa Magharibi haivumiliki tena kwa kadiri kwamba wakazi wa maeneo hayo wamenyimwa hata haki ya kutembea na kutoka eneo moja kwenda jingine.   

Maaskofu hao wamewataka Wakristo kote duniani kusali na kuwaombea wananchi wa Palestina wanaokandamizwa na utawala ghasibu wa Israel.