Bunge la Iraq: Wamarekani ondokeni haraka kutoka nchi hii
Naibu Spika wa Bunge la Iraq amepinga vikali uingiliaji wa kila mara wa ubalozi wa Marekani katika masuala ya ndani ya nchi hiyo ya Kiarabu na kusema, Washington inatakiwa kufanya haraka kuwaondoa askari wake kutoka Iraq.
Hassan Karim Al-Ka'abi amelaani vikali uingiliaji wa ubalozi wa Marekani katika masuala ya ndani ya Iraq na kusema kuwa, hivi sasa Washington inapanga njama chafu dhidi ya Iraq.
Itakumbukwa kuwa Jumatano iliyopita ubalozi wa Marekani mjini Baghdad ulitoa taarifa inayoingilia masuala ya serikali ya Iraq na kutaka kuzuia kile ulichokiita ukandamizaji wa waandamanaji katika mji wa Najaf.
Katika miezi ya hivi karibuni miji tofauti ya Iraq ukiwemo wa Najaf ilishuhudia maandamano ya wananchi wanaolalamikia hali mbaya ya huduma za kijamii, kukosekana kwa fursa za kazi na ufisadi wa kiidara. Hata hivyo katika wiki za hivi karibuni maandamano hayo yamegeuka kuwa ghasia na kusababisha makumi ya watu kuuawa na wengine kujeruhiwa. Nyaraka za kuaminika zinaonyesha kuwa maandamano nchini Iraq yanachochewa na nchi za kigeni.
Kufuatia hali hiyo Harakati ya Hizbullah ya Iraq hivi karibuni ilitangaza kuwa, serikali ya Marekani, utawala haramu wa Israel na baadhi ya tawala za Kiarabu ikiwemo Saudi Arabia na Imarati, zimehusika kuchochea ghasia na machafuko nchini Iraq, hasa baada ya pande hizo kutofurahishwa na siasa zinazotekelezwa na serikali ya Baghdad.
Hisia dhidi ya Marekani nchini Iraq zilishika kasi baada ya mwendelezo wa hatua za uhasama za Marekani dhidi ya nchi hiyo na muqawama hususan kitendo cha askari wa Kimarekani kumuua kigaidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) na Abu Mahdi al-Muhandis, Naibu Mkuu wa Harakati ya Wananchi ya Hashdu sh-Sha'abi ya Iraq.