Papa Francis akosoa mpango wa Trump wa Muamala wa Karne
(last modified Mon, 24 Feb 2020 04:40:37 GMT )
Feb 24, 2020 04:40 UTC
  • Papa Francis akosoa mpango wa Trump wa Muamala wa Karne

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, kwa njia isiyo ya moja kwa moja amekosoa mpango wa Rais Donald Trump wa Muamala wa Karne ambapo ameonya kuwa, mipango ya namna hiyo inayoegemea upande mmoja haiwezi kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Palestina na Israel.

Papa Francis amesema hayo leo Jumapili katika mji wa pwani wa Bari wa kusini mwa Italia wakati akifunga mkutano wa maaskofu wa eneo la Mediterranean na kusisitiza kuwa, mipango ya namna hiyo isiyozingatia masuala ya usawa haiwezi kuwa na matokeo mengine ghairi ya kushadidisha mgogoro uliopo au hata kuibua migogoro mipya.

Papa Fancis ameeleza bayana kuwa, "hatuwezi kufumbia macho mgogoro ambao haujatatuliwa wa Palestina na Israel. masuluhu yasiyo na usawa huenda yakapelekea kuibuka migogoro mipya." 

Hii ni mara ya kwanza kwa kiongozi  huyo wa Kanisa Katoliki Duniani kuzungumzia hadharani mgogoro wa Palestina na Israel, tangu Rais Donald Trump azindue rasmi mpango huo wa Muamala wa Karne unaokusudia kuwapokonya Wapalestina haki zao za msingi. 

Nchi mbalimbali duniani zimeandamana kulaani mpango huo wa Kimarekani-Kizayuni

Inafaa kuashiria hapa kuwa, tarehe 28 Januari, Rais Trump na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu walizindua mpango huo wa kibaguzi wa Muamala wa Karne katika Ikulu ya White House. 

Kwa mujibu wa mpango huo wa Marekani, Quds Tukufu itakabidhiwa kwa utawala wa Kizayuni; wakimbizi wa Kipalestina hawatakuwa na haki tena ya kurejea katika ardhi za mababu zao na makundi ya muqawama hayataruhusiwa kumiliki silaha. 

Tags