Wanaharakati: Mapambano Bahrain kuendelea hadi matakwa yatimizwe
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i5938-wanaharakati_mapambano_bahrain_kuendelea_hadi_matakwa_yatimizwe
Kiongozi wa mrengo wa Februari 14 nchini Bahrain amelaani wimbi la ukandamizaji na ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na utawala wa Aal-Khalifa dhidi ya wananchi na kusisitiza kuwa mapambano ya wapinzani yataendelea hadi matakwa yao yote yatakapotimizwa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 27, 2016 23:33 UTC
  • Wanaharakati: Mapambano Bahrain kuendelea hadi matakwa yatimizwe

Kiongozi wa mrengo wa Februari 14 nchini Bahrain amelaani wimbi la ukandamizaji na ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na utawala wa Aal-Khalifa dhidi ya wananchi na kusisitiza kuwa mapambano ya wapinzani yataendelea hadi matakwa yao yote yatakapotimizwa.

Rashid al-Rashid amesema wimbi la mwamko wa wananchi wa Bahrain litaendelea dhidi ya utawala wa kidekteta wa Manama licha ya vikosi vya usalama vya nchi hiyo ndogo ya Ghuba ya Uajemi kushadidisha hujuma za kulizima.

Kiongozi wa mrengo wa Februari 14 ameliambia shirika la habari la Tasnim kuwa, utawala wa Bahrain umeomba msaada wa kijeshi kutoka Marekani, Uingereza, Ufaransa, Jordan na Saudi Arabia kwa lengo la kuwasaidia katika juhudi zao za kuzima mapambano ya wananchi.

Hadi sasa maelfu ya wanaharakati na viongozi wa kidini akiwemo Sheik Ali Salman, Katibu Mkuu wa harakati ya Kiislamu ya Al-Wifaq, wanaendelea kushikiliwa katika korokoro za utawala huo wa Bahrain mbele ya kimya cha jamii ya kimataifa.

Hata hivyo na pamoja na ukandamizaji huo, maandamano dhidi ya utawala huo yameendelea kushuhudiwa katika maeneo tofauti ya utawala huo kibaraka wa Saudi Arabia.