Vita vya madaraka vya pande kadhaa vya Bin Salman
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i59686-vita_vya_madaraka_vya_pande_kadhaa_vya_bin_salman
Mohammad bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia ameanzisha vita vikubwa vya madaraka kuanzia ndani hadi nje ya nchi hiyo ya utawala wa kiukoo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 11, 2020 23:11 UTC
  • Vita vya madaraka vya pande kadhaa vya Bin Salman

Mohammad bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia ameanzisha vita vikubwa vya madaraka kuanzia ndani hadi nje ya nchi hiyo ya utawala wa kiukoo.

Kwa vitendo vyake mbalimbali, Mohammad bin Salman ameonesha wazi kuwa ana maradhi ya uchu wa madaraka na hivi sasa anapigana kufa na kupona kukikalia kiti cha ufalme wa Saudi Arabia. Bin Salman ndiye aliye na nafasi kubwa ya kutwaa kiti hicho kutokana na hali isiyo nzuri ya kiafya ya baba yake mzee na mgonjwa; Salman bin Abdulaziz  mwenye umri wa miaka 85. Hadi hivi sasa bin Salman ameshachukua hatua kadha za kuhakikisha hana mpinzani katika kukikalia kiti cha ufalme huko Saudia.

Hatua ya kwanza ni kuleta marekebisho nchini Saudi Arabia. Mrithi huyo kijana wa kiti cha ufalme wa Saudia, nchi isiyoelewa kabisa neno demokrasia, aligaiwa cheo hicho na baba yake mwaka 2017 na tangu wakati huo amekuwa akichukua hatua mbalimbali za kubadilisha mfumo wa kijamii na kiutamaduni na hasa katika suala la wanawake na uhuru wa watu kupiga muziki na kunengua majukwaani wanavyotaka nchini humo. Kwa hatua zake hizo zilizo kinyume na Uislamu, bin Salman alitaka kupata uungaji mkono wa wanawake na vijana bila ya kujali madhara makubwa na uharibifu wake huo.

Mohammed bin Nayef, mrithi wa zamani wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia aliyepokonywa na kupewa Mohammad bin Salman

 

Hatua ya pili muhimu iliyochukuliwa na kijana huyo ni kushadidisha ukandamizaji wa kisiasa ndani ya Saudi Arabia. Sambamba na mabadiliko ya kiutamaduni na kufungua milango ya vitendo vingi zaidi vya ufuska huko Saudia, bin Salman ameanzisha pia wimbi kubwa la ukandamizaji ikiwa ni pamoja na kuwatia mbaroni na kuwaweka korokoroni makumi ya wana wa wafalme wa nchi hiyo kama njia ya kufukia na kushindilia chini upinzani wowote dhidi yake. Hata hivyo inaonekana ukandamizaji huo haukumsaidia sana bin Salman kwani miaka miwili baada ya wimbi hilo la kwanza la kuwatia mbaroni wana wafalme, hivi sasa pia mrithi huyo wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia ameanzisha wimbi jingine la kutiwa mbaroni watu wa ukoo wa kifalme. Waliotangazwa kutiwa mbaroni mara hii huko Saudi Arabia ni wana wafalme 20 akiwemo Ahmad bin Abdulaziz, ami yake bin Salman, yaani ndugu wa kiume wa baba yake. Mwengine aliyetiwa mbaroni ni Mohammad bin Nayef, aliyekuwa mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia ambaye alipokonywa cheo hicho na kupewa bin Salman. 

Mohammad Rezai ni mtaalamu wa masuala ya Saudi Arabia. Mtazamo wake yeye ni kwamba kuna uhusiano wa moja kwa moja baina ya marekebisho yanyofanywa na bin Salman na siasa za kutiwa mbaroni wapinzani wake. Anasema, inabidi kuunganishwa moja kwa moja siasa za kutiwa mbaroni wapinzani wa bin Salman na siasa zake za mabadiliko ya kiutamaduni ndani ya Saudia. Mchambuzi huyo anaamini kwamba, mabadiliko yanayofanywa na bin Salman nchini Saudi Arabia ni kutokea juu kwendea chini sawa kabisa na mbinu iliyotumiwa na Ataturk wakati alipokuwa anaendesha kampeni za kuufuta Uislamu nchini Uturuki. Mbinu hiyo inahitajia nguvu za ziada, ukandamizaji na mkono wa chuma kuitekeleza. 

Shirika la Taifa la Mafuta la Saudi Arabia (ARAMCO) baada ya kuchakazwa na mashambulizi ya kujihami ya wanamapambano wa Yemen

 

Amma suala jingine lililopo hapa ni kwamba, ndoto za bin Salman haziishii tu ndani ya Saudia, bali siasa zake zimeota mbawa na kufika hadi nje ya nchi hiyo. Kumwaga mapesa mengi ya mafuta katika kuingilia masuala ya nchi nyingine kama vile Iran, Syria, Iraq, Misri, Libya, Tunisia, Bahrain na kwengineko na kuanzisha vita vya kikatili dhidi ya wananchi maskini wa Yemen ni katika sera za Saudia zilizoshika kasi kwa amri ya Mohammad bin Salman. Si hayo tu, lakini pia Saudi Arabia imeanzisha vita vya mafuta dhidi ya Russia. Hivi karibuni Russia imekataa kupunguza kiwango chake cha kuzalisha mafuta wakati Saudia ilishikilia jambo hilo kama njia ya kupandisha bei ya bidhaa hiyo au kwa uchache kuthibiti isizidi kushuka.

Kitendo cha Russia cha kukataa kupunguza kiwango cha uzalishaji wake wa mafuta kimeikasirisha Saudia na kuamua kuchukua hatua za kuporomosha kabisa bei ya mafuta. Hatua hiyo inahesabiwa kuwa ni vita vipya vya mafuta vilivyoanzisha na Saudi Arabia dhidi ya Russia. Hata hivyo kwa hatua yao hiyo, viongozi wa Riyadh wameonywa kwamba wanacheza mchezo wa "pata potea" kwani hisa za shirika kuu la mafuta la Saudi Arabia (ARAMCO) zimepungua sana huku virusi vya corona vikienea nchini Saudia na kuilazimisha nchi hiyo kusimamisha amali za Umra na Hijja ambazo ni katika sekta zinazoiingizia fedha nyingi za kigeni nchi hiyo.

Alaakullihaal, inavyoonekana ni kwamba wimbi la kutiwa mbaroni watu litaendelea huko Saudi Arabia hasa kutokana na uzoefu wa huko nyuma kuonesha kuwa Mohammad bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa nchi hiyo, hana kifua cha kuvumilia wapinzani wake, si wa ndani tu, bali hata wa nje ya Saudia.