Palestina yamwandikia barua Guterres, yatahadharisha kuhusu ujenzi wa vitongoji vya Wazayuni
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i59751-palestina_yamwandikia_barua_guterres_yatahadharisha_kuhusu_ujenzi_wa_vitongoji_vya_wazayuni
Mwakilishi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa amewatahadharisha maafisa wa umoja huo kuhusu kasi ya ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika Ardhi ya Palestina na uchochezi unaofanywa na utawala huo dhidi ya raia wa Palestina.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 15, 2020 00:48 UTC
  • Riyadh al Maliki
    Riyadh al Maliki

Mwakilishi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa amewatahadharisha maafisa wa umoja huo kuhusu kasi ya ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika Ardhi ya Palestina na uchochezi unaofanywa na utawala huo dhidi ya raia wa Palestina.

Riyadh al Maliki amemwandikia barua Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, mwakilishi wa China katika Umoja huo ambaye ndiye Mwenyekiti wa sasa wa Baraza la Usalama na vilevile Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Tijjani Muhammad-Bande akitahadharisha kuhusu kasi ya ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu huko Palestina.

Al Maliki ameashiria mpango wa Israel wa kujenga nyumba 1,736 katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na kutahadharisha kwamba, utawala huo haramu unafanya mipango ya kujenga vitongoji zaidi vya walowezi katika ardhi ya Ukingo wa Magharibi.

Ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni huko Palestina

Mwakilishi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa ametahadharisha kuhusu mipango ya sasa ya Israel ya kutumia vibaya kipindi hiki ambapo dunia nzima imeelekeza mazingatio yake katika janga la Corona kwa ajili ya kutwaa na kupora ardhi zaidi za Palestina na kusema hatua hiyo inakiuka sheria za kimataifa.

Utawala wa Kizayuni wa Israel umeendelea kupuuza maazimio ya Umoja wa Mataifa na kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika eneo la Quds Mashariki na Ukingo wa Magharibi.