Hamas yaziomba taasisi za kimataifa ziwasaidie mateka wa Kipalestina
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, imeziomba taasisi za kisheria za kimataifa zichukua hatua za kuwanusuru mateka wa Kipalestina katika jela za utawala wa Kizayuni waq Israel kutokana na kukithiri maambukizo ya virusi vya corona katika jela hizo.
Msemaji wa harakati ya Hamas, Abdullatif al Qanou amesema kuwa kitendo cha taasisi inayosimamia jela za utawala wa Israel cha kuzuia hatua za kudhibiti maambukizi ya corona na wakati huo huo kuzuia kuingizwa dawa za kujikinga na maambukizo katika jela hizo ni jinai dhidi ya binadamu.
Wakati huo huo Harakati ya Wafungwa wa Palestina pia imesisitiza kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel unazuia wafungwa wa Kipalestina wasipewe vifaa vya dharura zikiwemo dawa na vifaa vya afya vya kujikinga na maambukizo ya virusi vya corona.
Vilevile Kamati ya Masuala ya Wafungwa wa Kipalestina wiki iliyopita ilitangaza kuwa, utawala wa Kizayuni ulimtuma mgonjwa mmoja raia wa Palestina katika jela ya Asqalan kwa daktari wa Kiisraeili ambaye alikuwa ameathiriwa na virusi vya corona kwa ajili ya kupatiwa matibabu. Baada ya kurejea jela mateka huyo wa Kipalestina aliamiliana na idadi kubwa ya wafungwa ndani ya jela hiyo na kuna uwezekano ameeneza maambukizo kwa watu wengine wengi.