Mauaji ya askari zaidi wa Uturuki nchini Syria
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i59885-mauaji_ya_askari_zaidi_wa_uturuki_nchini_syria
Wizara ya Uinzi ya Uturuki imetangaza kuwa, wanajeshi wengine wawili wa nchi hiyo wameuawa katika mkoa wa Idlib nchini Syria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 21, 2020 22:02 UTC
  • Mauaji ya askari zaidi wa Uturuki nchini Syria

Wizara ya Uinzi ya Uturuki imetangaza kuwa, wanajeshi wengine wawili wa nchi hiyo wameuawa katika mkoa wa Idlib nchini Syria.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Ulinzi ya Uturuki imesema kuwa, wanajeshi hao wawili wameuawa katika shambulizi la roketi lililolenga ngome za jeshi la nchi hiyo katika mkoa wa Idlib na kwamba mwanajeshi mwingine amejeruhiwa. Baada ya mauaji hayo jeshi la Uturuki na wanamgambo wanaosaidiwa na nchi hiyo wameshambulia vijiji kadhaa vya mkoa wa Idlib huko kaskazini mwa Syria. 

Katika wiki za hivi karibuni makumi ya wanajeshi wa Uturuki wameuawa katika ardhi ya kaskazini na kaskazini magharibi mwa Syria. 

Serikali ya Syria ilianzisha operesheni kubwa ya kusafisha maeneo hayo ya mkoa wa Idlib na kuwafurusha magaidi katika maeneo hayo miezi miwili iliyopita. Hata hivyo Uturuki ambayo inapinga hatua hiyo, imevamia sehemu ya ardhi ya Syria kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi.

Tajiriba ya Uturuki huko kaskazini mwa Syria inaonyesha kuwa, nchi hiyo haina stratijia madhubuti ya kushughulikia masuala ambayo Rais Recep Tayyep Erdogan anadai kuwa yanatishia usalama wa Uturuki. Hatua za Uturuki nchini Syria zimeibua vitisho ambavyo sasa Ankara inadai inataka kuvishughulikia. 

Rais Recep Tayyep Erdogan wa Uturuki  

Wachambuzi wa mambo wanajua vyema kwamba, kujitokeza kwa makundi ya waasi wa Kikurdi huko kaskazini mwa Syria kulitokana na hatua na sera za serikali ya Uturuki za kuanzisha mgogoro dhidi ya serikali ya Damascus. Suala hilo lilikuwa sababu ya kuondoa udhibiti wa eneo la kaskazini mwa Syria mikononi mwa serikali ya Damasus na kutengeza ombwe la kiutawala na hatimaye kuibuka makundi ya waasi.

Vilevile Uturuki, badala ya kutafuta suluhisho la kimantiki la matatizo yake, imewaunga mkono waasi na wanamgambo wa Kikurdi kwa shabaha ya kutimiza malengo yake kupitia njia ya kufanya mauaji ya kimbari huko kaskazini mwa Syria.

Hii ni pamoja na kuwa, sera za Erdogan na misaada na uungaji mkono wake kwa makundi ya kigaidi kama Daesh ambao uliodhihirika wazi zaidi kwa walimwengu katika eneo la Kobani, vimekuwa kisingizio kilichotumiwa na Marekani kutuma majeshi huko kaskazini mwa Syria na kuikalia kwa mabavu ardhi ya nchi hiyo.

Kwa sasa inaonekana kuwa Rais huyo wa Uturuki anataka kubakisha majeshi ya nchi yake katika ardhi ya Syria kwa malengo ya muda mrefu ya kuvamia huko mashariki mwa Furati. Hata hivyo Erdogan amefumbia macho uhakika wa kuendelea kusambaratika makundi ya kigaidi huko kaskazini mwa Syria ambapo iwapo Ankara haitatia kiguru chake kuzuia operesheni ya jeshi la Syria, watasalimu amri na kuinua mikono juu haraka iwezekanavyo.

Magaidi kaskazini mwa Syria  

Alaa kulli hal, tunaweza kusema kuwa, stratijia inayotumiwa sasa na Uturuki huko Syria imekuwa sababu ya kuanikwa na kuwekwa wazi sera zisizofaa za serikali ya Ankara na hapana shaka kuwa, kuuliwa wanajeshi zaidi wa nchi hiyo huko Syria kunazidisha gharama za moja kwa moja za uingiliaji wa nchi hiyo katika masuala ya nchi jirani. Hivyo hapana shaka kuwa, Rais Recep Tayyep Erdogan hataweza kutetea na kuhalalisha tena mashambulizi ya nchi hiyo huko Syria kwa kipindi kirefu ambayo yanapelekea kuuawa idadi kubwa ya wanajeshi wa nchi hiyo. Hali hii pia itapelekea kutengwa zaidi Erdogan katika kanda hii ya magharibi mwa Asia.

Siasa za ndani za Uturuki zinaonyesha kwamba, sera za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja za chama cha Uadilifu na Ustawi cha Recep Tayyep Erdogan zimepelekea kupungua umashuhuri wa chama hicho baina ya Waturuki. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, wapinzani wa chama hicho wametumia udhaifu huo na kukitimulia vumbi katika uchaguzi wa serikali za mitaa.

Kwa msingi huo Erdogan anapaswa kutilia maanani masuala ya ndani ya nchi yake na kurekebisha sera na siasa zake za nje la sivyo atajikuta nje ya ulingo wa siasa za Uturuki.