HAMAS yatoa onyo kali kwa utawala wa Kizayuni wa Israel
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imesisitiza kuwa, mashambulizi ya utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Ghaza yatazidi kuufanya muqawama ushikilie msimamo wake wa kupinga njama za Israel za kuteka ardhi zaidi za Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Shirika la habari la IRNA limemnukuu Msemaji wa HAMAS, Hazim Qasim akisema hayo leo kujibu mashambulio mapya ya ndege za Israel katika Ukanda wa Ghaza na kusisitiza kuwa kuna wajibu wa kuendelea na muqawama wa kukabiliana na maadui na kwamba uvamizi huo mpya wa Wazayuni huko Ghaza utazidi tu kuifanya imara misimamo ya wananchi wa Palestina ya kupigania haki zao na kupinga kutekwa ardhi zao zaidi za Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Amesema, jinai mpya za Wazayuni za kuushambulia Ukanda wa Ghaza ni kuzidi kuonesha ukubwa wa uadui wa utawala huo pandikizi unaozikalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina zikiwemo zile za mji mtakatifu wa Quds.
Jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel usiku wa kuamkia leo Jumamosi zimefanya mashambulizi katika Ukanda wa Ghaza.
Hapo kabla, Abu Ubaida, Msemaji wa Brigedi za Ezzedin Qassam, Tawi la Kijeshi la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, alitangaza kuwa makundi ya muqawama na ya kupigania ukombozi wa Paletina yataufanya utawala wa Kizayuni ujute kukalia kwa mabavu maeneo zaidi ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Abu Ubaida ametoa tamko hilo baada ya wakuu wa Marekani kutangaza kuwa rais wa nchi hiyo Donald Trump anatazamiwa kuzindua mpango mpya kuhusu Palestina.