China: Uvamizi na uhasama dhidi ya Palestina haupaswi kuhalalishwa
Waziri wa Mambo ya Nje wa China ameashiria kuhusu uungaji mkono wa nchi hiyo ya Asia kwa wananchi madhulumu wa Palestina na kusisitiza kuwa, kuhujumiwa haki za msingi za Wapalestina hakupaswi kuhalalishwa.
Wang Yi amesema hayo katika Mkutano wa Ushirikiano wa China na nchi za Kiarabu uliofanyika kwa njia ya intaneti na kueleza bayana kuwa, takwa la kihistoria la wananchi wa Palestina la kuheshimiwa haki zao halipaswi kuendelea kupuuzwa.
Amegusia kuhusu mpango wa utawala haramu wa Israel wa kulitwaa eneo la Ukingo wa Magharibi na kuliunganisha na maeneo mengine ya Palestina yaliyoghusubiwa na utawala huo na kusema: Uvamizi dhidi ya Palestina haupaswi kuhalalishwa.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa China amekumbusha kuwa, haki za msingi za Wapalestina zinapaswa kuheshimiwa na kwamba China itaendelea kusimama na kuliunga mkono taifa hilo madhulumu.
Utawala haramu wa Kizayuni wa Israel ulikuwa umepanga kwamba Jumatano iliyopita ya tarehe Mosi Julai ungeanza kutekeleza mpango wake haramu wa kupora na kuunganisha asilimia 30 ya ardhi za Ukingo wa Magharibi na ardhi nyingine za Palestina unazozikalia kwa mabavu.
Hata hivyo umelazimika kuakhirisha tarehe ya utekelezaji wa mpango huo baada ya kushadidi mashinikizo ya upinzani ya Wapalestina na ya nchi mbalimbali duniani. Mpango huo ni sehemu ya mapendekezo ya Rais Donald Trump wa Marekani yaliyowekwa katika kile kinachodaiwa ni "Muamala wa Karne".