Hizbullah: Katika kamusi yetu hakuna kitu kinachoitwa 'kusalimu amri'
Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon amesisitiza kuwa, harakati hiyo pamoja na washirika wake hawataruhusu Marekani na vibaraka wake waitumbukize Lebanon katika ombwe la uongozi na mzozo wa kisiasa.
Sheikh Naim Qassim amesema kuwa, katika kipindi chote cha historia Hizbullah imekuwa na chaguo moja kati ya machaguo mawili ima kupata ushindi au kufa shahidi na kwamba, katika kamusi ya harakati hiyo hakuna kitu kinachoitwa kusalimu amri.
Aidha amesema kuwa, Hizbullah ya Lebanon imejiandaa kikamilifu kiasi kwamba, ina uwezo wa kuzuia machaguo na mipango ya wengine inayolenga kuitwisha mambo harakati hiyo.
Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon amesema pia kuwa, vita vya sasa ni vita vya kiuchumi ambavyo vimechuikua nafasi ya vita vya kijeshi na kimsingi vita hivi vimeanzishwa na Marekiani na utawala ghasibu wa Israel.
Sheikh Naim Qassim amesema bayana pia kwamba, endapo kutaibuka vita na utawala haramu wa Israel bila shaka utawala huo ndio utakaoshindwa; kwani nguvu ya muqawama hii leo ni kubwa mno ikilinganishwa na vita vya siku 33 vilivyotokea mwaka 2006 na Tel-Aviv inafahamu vyema jambo hilo.
Kiongozi huyo wa ngazi za juu wa wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon ameongeza kuwa, lengo la Marekani kuweko katika eneo la Asia Magharibi ni kuuunga mkono utawala ghasibu wa Israel na kusaidia kupokonya haki za wananchi madhulumu wa Palestina.