Amnesty yaitaka Saudia imwachie huru mwakilishi wa Hamas na mwanawe
(last modified Fri, 21 Aug 2020 11:45:23 GMT )
Aug 21, 2020 11:45 UTC
  • Dr Mohammad Al-Khodari
    Dr Mohammad Al-Khodari

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty international limeeleza wasiwasi wake kuhusu afya ya mwakilishi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, HAMAS, anayeshikiliwa jela nchini Saudi Arabia akisumbuliwa na ugonjwa wa saratani.

Taarifa iliyotolewa na Amnesty International imesema kuwa, mwakilishi wa Hamas mwenye umri wa miaka 81 nchini Saudia, Dr Mohammad Al-Khodari na mtoto wake, Hani, wanashikiliwa jela Saudi Arabia kwa kipindi cha mwaka mmoja sasa na wamezuiwa kukutana na wakili na mwanasheria wao. 

Amnesty International imesema kuwa: Haki za binadamu za Wapalestina hao wawili zinakanyagwa, ikiwa ni pamoja na kukamatwa kidhalimu na kukatiwa mawasiliano yote na dunia katika seli ya mtu mmoja wanakoshikiliwa. 

Taarifa ya Amnesty Intenational imesema kuwa, maradhi ya saratani ya Dr Mohammad Al-Khodari yanamuweka katika hatari ya kupatwa na virusi vya corona; kwa msingi huo anahitajia uangalizi wa madaktari na tiba ya kansa. 

Al Khodari amekuwa mwakilishi rasmi wa Hamas nchini Saudi Arabia kwa muda wa miaka 25 na alitiwa nguvuni na maafisa wa utawaka huo Aprili mwaka 2019. Saudi Arabia pia imemkamata mtoto wake, Hani al Khodari. 

Amnesty International inasema Saudi Arabia inawashikia jela wanafunzi wa vyuo vikuu, wasomi, wafanyabiashara na mahujaji bila ya kuwafikisha mahakamani. Mahabusu hao wamekatiwa mawasiliano yote na dunia na hawaruhusiwi kukutana wala kuwasiliana na familia na mawakili wao. Mali za mahabusu hao pia zimetwaliwa na serikali ya Riyadh.  

Tags