Hamas yakanusha madai ya kukamatwa wanachama wake 2 na Marekani
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imekadhibisha vikali madai kwamba Marekani imewatia mbaroni watu wawili wenye mfungamano na harakati hiyo.
Shirika la habari la Shahab la Palestina limenukuu taarifa ya Hamas ikikanusha vikali madai hayo na kusisitiza kuwa haiwatambui wala haina uhusiano wowote na watu wawili waliokamatwa na Marekani.
Siku ya Alkhamisi, Wizara ya Sheria ya Marekani ilitangaza kuwa imewakamata wanachama wawili wa kundi lenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia na lililo dhidi ya serikali la Boogaloo Bois.
Washington ilidai kuwa, wawili hao Michael Robert Solomon, 30, na Benjamin Ryan Teeter, 22 wamekamatwa kwa madai ya kula njama ya kuipa misaada ya kifedha harakati ya Hamas. Hamas imetupilia mbali tuhuma hizo na kueleza bayana kuwa, haiwafahamu wala haina uhusiano wowote na wawili hao waliokamatwa na Marekani.
Taarifa ya Hamas imesisitiza kuwa, harakati hiyo ya muqawama inapigania ukombozi wa Wapalestina mkabala wa utawala ghasibu wa Israel, na katu haiingilii masuala ya ndani ya nchi nyingine.
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina imesema madai hayo ya Washington ni sehemu ya mpango maalumu wenye lengo la kuzima ari na muqawama wa Wapalestina, na kampeni ya kutafuta uungaji mkono zaidi kutoka kwa lobi za Kizayuni, kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu 2020 nchini Marekani.