Haniya: Marekani inajaribu kuanzisha njia za mazungumzo na Hamas
Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) amesema Marekani imefungua njia za kuanzisha mazungumzo na maafisa wa ngazi za juu wa harakati hiyo, ili kulishawishi kundi hilo liafiki kutekeleza mpango wa 'Muamala wa Karne.'
Ismail Haniya ameashiria kuhusu ujumbe wa Jared Kushner, mkwe na mshauri mkuu wa Rais Donald Trump wa Marekani kwa harakati hiyo na kubainisha kuwa: Ofisi ya Kushner imeviomba baadhi ya vyama na makundi kuzungumza na maafisa wa ngazi za juu wa harakati ya Hamas, na wametutumia ujumbe juu ya kadhia hiyo. Wapo tayari kukutana na sisi popote pale, ama katika mji mkuu wa moja ya nchi za Kiarabu au Ulaya kujadili hali ya Ghaza."
Haniya amesisitiza kuwa, harakati hiyo ya muqawama haina tatizo kufanya mazungumzo na nchi yoyote ile duniani, lakini inapinga kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Amesema utawala haramu wa Israel umeshindwa kuipokonya silaha na kuizingira harakati ya Hamas licha ya jitihada zake za kuanzisha uhusiano wa kawaida na baadhi ya nchi za Kiarabu, mbali na kuiweka harakati hiyo katika orodha yake ya makundi ya kigaidi. Ameeleza bayana kuwa, licha ya njama zote hizo, lakini mrengo wa muqawama umeendelea kuimarika na kupanuka.
Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) ameongeza kuwa: Sisi hatufuatilii kuanzisha vita Ghaza, lakini pia hatuviogopi. Iwapo utawala ghasibu utafikiria kufanya uvamizi mpya dhidi ya ukanda huo, vita vitakuwa tofauti kabisa, kwa kuwa makundi ya Palestina pamoja na Brigedi ya Izzuddin Qassam yana zana za kisasa zitakazoushangaza utawala wa Kizayuni.
Ili kufanikisha njama dhidi ya Wapalestina zilizopewa jina la 'Muamala wa Karne' tayari Imarati na Bahrain zimetangaza kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel, makubaliano ambayo yamekabiliwa na wimbi kali la malalamiko na upinzani wa makundi ya Palestina, nchi za Kiislamu katika eneo la Asia Magharibi na shakhsia kadhaa wa kisiasa, kijamii na kidini kote duniani.