Saudia kupokea mahujaji wa ibada ya Umra mwezi mmoja ujao
Serikali ya Saudi Arabia imetangaza kuwa itaanza kupokea mahujaji wa kigeni wa Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya ibada ya Umra mwezi mmoja ujao baada ya ibada hiyo kusitishwa kwa miezi 8.
Waziri wa Hija na Umra wa Saudi Arabia, Mohammad Saleh Benten amesema, baada ya miezi 8 ya kusitisha kupokea mahujaji katika miji ya Makka na Madina kutokana na maambukizi ya virusi vya corona, kuanzia leo Jumapili mahujaji wa ibada ya Umra kutoka ndani ya nchi, na mwezi mmoja baadaye mahujaji kutoka nje ya Saudia wataruhusiwa kufanya Umra lakini kwa kuzingatia masharti.
Waziri wa Hija na Umra wa Saudia ameongeza kuwa, katika awamu ya kwanza Waislamu elfu 6 wataruhusiwa kuingia Saudi Arabia kwa ajili ya kutekeleza ibada ya Umra katika kipindi makhsusi na kifupi, na wataruhusiwa kuingia Msikiti mtakatifu wa Makka katika kalibu ya makundi madogo madogo.
Ripoti ya Wizara ya Hija ya Saudia inasema, imepangwa kuwa hadi tarehe 18 Oktoba idadi ya mahujaji wa ibada ya Umra itaongezeka na kufikia elfu 15, na watu elfu 45 wataruhusiwa kutekeleza Swala ndani ya Masjidul Haram. Ripoti hiyo inasema kuwa, kuanzia mwezi Novemba ambapo mahujaji wa kigeni wataruhusiwa kuingia Makka, idadi ya mahujaji itaongezeka na kufikia elfu 20 na watu elfu 60 wataruhusiwa kutekeleza Swala ndani ya Masjidul Haram.
Mwaka jana Waislamu milioni mbili na nusu walitekeleza ibada ya Hija nchini Saudi Arabia.
Takwimu rasmi zinaonyesha kuwa mwaka jana wa 2019 serikali ya Saudi Arabia ilikusanya dola bilioni 12 kutokana na ibada ya Hija na watalii wa kidini.