Hamas: Waandishi wa habari wasiupe jukwaa utawala wa Kizayuni wa Israel
Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) amewakosoa waandishi wa habari hususan katika nchi za Kiarabu kwa kumpa waziri wa vita wa Israel jukwaa la kuhubiri siasa na sera za utawala huo haramu.
Matamshi hayo ya msemaji wa Hamas yametolewa baada ya waandishi wa habari wa nchi za Saudi Arabia, Imarati na Bahrain kufanya mahojiano na waziri wa vita wa Israel, Benny Gantz kupitia ntandao wa intaneti.
Msemaji wa Hamas, Hazem Qasem amesema Benny Gantz amesababisha mauaji ya raia wasio na hatia wa Palestina na ni mtenda jinai za kivita.
Hazem Qasem amesema kuwa, ni jambo baya sana kwa mwandishi wa habari wa Kiarabu kutangaza mitazamo ya viongozi wa utawala haramu wa Israel na kwamba jambo hilo lina madhara kwa riwaya sahihi na ya kweli ya Wapalestina, na linaeneza riwaya ya uongozo na isiyo sahihi ya utawala bandia wa Israel.
Itakumbukwa kuwa tarehe 15 mwezi uliopita wa Septemba nchi za Imarati na Bahrain zilisaini mapatano ya kuanzisha uhusiano rasmi na utawala haramu wa Israel katika sherehe iliyofanyika White House nchini Marekani. Mapatano hayo yametambuliwa na Wislamu kuwa ni usaliti mkubwa wa mapambano ya kupigania uhuru ya watu wa Palestina.