UN yatoa ripoti kuhusu jinai za muungano wa Saudia nchini Yemen
Kamisheni Kuu ya Wakimbizi ya Umoja wa Mataifa imetoa ripoti ya jinai kubwa za muungano vamizi wa Saudi Arabia huko Yemen na kutangaza habari ya kuuawa na kujeruhiwa zaidi ya raia 1,500 katika mashambulio yao ya kikatili huko Yemen.
Mtandao wa habari wa Middle East Eye umeripoti habari hiyo na kunukuu taarifa iliyotolewa jana (Jumatano) katika ripoti ya Kamisheni Kuu ya Wakimbizi ya Umoja wa Mataifa na kuongeza kuwa, tangu mwezi Januari hadi Septemba 2020, Saudia na kundi lake limeua na kujeruhi raia na watu wa kawaida zaidi ya 1,500 nchini Yemen.
Katika ripoti hiyo iliyowekwa kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter, Kamisheni Kuu ya Wakimbizi ya Umoja wa Mataifa vile vile imesema, asilimia 42 ya wahanga wa mauaji hayo ya kikatili ya muungano wa Saudi Arabia, ni wanawake na watoto wadogo wa Yemen.
Saudi Arabia kwa kushirikiana na Umoja wa Falme za Kiarabu na baadhi ya nchi nyingine, zilianzisha mashambulizi ya kivamizi ya pande zote dhidi ya nchi maskini ya Kiarabu na Kiislamu ya Yemen, mwezi Machi 2015 kwa tamaa ya kumaliza haraka vita hivyo na kuziteka ardhi zote za nchi hiyo.
Madai yaliyotolewa na wavamizi hao wanaofanya jinai kubwa dhidi ya Waislamu wa Yemen kwa silaha wanazopewa na madola ya kibeberu ya Magharibi na utawala wa Kizayuni wa Israel, yalikuwa ni kuirejesha madarakani serikali ya Abdul Hadi Mansour Hadi, rais wa zamani wa Yemen aliyejiuzulu na kukimbilia Saudi Arabia.
Hata hivyo muqawama wa kupigiwa mfano wa wananchi wa Yemen umefelisha ndoto za wavamizi hao ambao hadi sasa wameshaua kidhulma zaidi ya Wayemen 16,000, kujeruhi makumi ya maelfu na kuwafanya wakimbizi mamilioni ya Wayemen wengine.