Imarati na Israel zashirikiana kurejesha magaidi kusini mwa Syria
Vyombo vya usalama vimefichua kwamba, Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) umetuma ujumbe wa taasisi za upelelezi na ujasusi huko Israel kwa ajili ya kuchunguza mpango wa kurejesha makundi ya kigaidi katika miji ya kusini mwa Syria inayopakana na ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni za Palestina.
Vyombo hivyo vimefichua kuwa, ili kutekeleza mpango huo, utawala ghasibu wa Israel na Imarati zimeazimia kuanzisha kundi la kijeshi kwa jina la wapinzani wa serikali ya Syria.
Vyombo hivyo vimeongeza kuwa, hatua hiyo ya Imarati inafanyika katika fremu ya stratijia ya kijeshi ya Abu Dhabi nchini Syria, na kwa sababu hiyo vinara wa zamani wa makundi ya upinzani ya Syria wanatumiwa kwa ajili ya kufanikisha njama hiyo.
Utawala wa Kizayuni wa Israel daima umekuwa ukiyafadhili na kuyaunga mkono makundi ya kigaidi kwa ajili ya kuzusha ghasia na machafuko katika maeneo ya kusini mwa Syria.
Tarehe 15 Septemba mwaka huu Imarati ilisaini mapatano ya kuanzisha rasmi uhusiano wa kidiplomasia na utawala haramu wa Israel unaoendelea kukalia kwa mabavu ardhi ya Palestina na kibla cha kwanza cha Waislamu.
Hatua hiyo iliyosimamiwa na Marekani, imepingwa vikali baina ya mataifa ya Kiislamu yaliyotaja kuwa ni kusaliti mapambano ya ukombozi ya Palestina.