Iraq: Tunaiunga mkono Palestina, hatuna mpango wa kupatana na Israel
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq amesisitiza kuwa, nchi yake itaendelea kuliunga mkono taifa la Palestina na kwamba suala la kupatana na Wazayuni halina nafasi kabisa katika siasa za nchi hiyo.
Shirika la habari la FARS limenukuu Fuad Hussein akisema hayo akiwa ziarani mjini Moscow, Russia, na kusisitiza kuwa, wananchi wa Iraq wanaliunga mkono taifa la Palestina na kwamba hakuna mpango wowote wa kuwa na mapatano na Wazayuni wala kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel.
Amesema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa na shirika la habari la Sputnik na kusema: Kuhusu kadhia ya Palestina jamii ya wananchi wa Iraq inatofautiana na jamii nyinginezo kwani kwa taifa la Iraq, suala la Palestina si sehemu ya siasa za kigeni tu, bali ni sehemu muhimu ya siasa za ndani ya Iraq na linawahusu moja kwa moja wananchi wa nchi hiyo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq vile vile amesema, jamii ya Iraq ni ya watu walioshikamana na malengo matukufu ya Palestina na wanaitakidi ndani ya nyoyo zao kwamba Wapalestina wameporwa haki zao na wana haki ya kusimama kidete kupigania ukombozi na kujiamulia wenyewe mustakbali wanaoutaka.
Aidha amesema, katika mazungumzo yake na viongozi wa Russia, nchi mbili zimejadiliana hali ya kiusalama na kijeshi ya nchi yake na inatarajiwa kwamba karibuni hivi Waziri wa Ulinzi wa Iraq, Juma Inad, atafanya ziara mjini Moscow.
Vile vile amesema ameelekea mjini Moscow kwa mwaliko rasmi wa waziri mwenzake wa mambo ya nje wa Russia, Sergey Lavrov.
Amma kuhusiana na Iraq kununua silaha za Russia, Fuad Hussein amesema, suala hilo halikujadiliwa katika mazungumzo yake na viongozi wa Moscow, bali kilichojadiliwa zaidi ni hati ya maelewano baina ya nchi mbili.