Mufti wa ISIS: Niliitembelea Saudia mara mbili kukusanya pesa
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i64925-mufti_wa_isis_niliitembelea_saudia_mara_mbili_kukusanya_pesa
Mufti wa genge la kigaidi la Daesh (ISIS) huko kaskazini mwa Iraq amefichua kuwa, aliwahi kutembelea mara mbili Saudi Arabia kwa ajili ya kukusanya fedha za vitendo vya kigaidi vya genge hilo la ukufurishaji.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 30, 2020 03:34 UTC
  • Mufti wa ISIS: Niliitembelea Saudia mara mbili kukusanya pesa

Mufti wa genge la kigaidi la Daesh (ISIS) huko kaskazini mwa Iraq amefichua kuwa, aliwahi kutembelea mara mbili Saudi Arabia kwa ajili ya kukusanya fedha za vitendo vya kigaidi vya genge hilo la ukufurishaji.

Shifaa al Nima ambaye pia alikuwa jaji wa mahakama ya genge la kigaidi la Daesh katika mkoa wa Nainawa (Nineve) wa kaskazini mwa Iraq, jana Jumapili alitoa ufafanuzi zaidi kuhusu Wasaudia wanavyoliunga mkono genge la kigaidi la ISIS nchini Iraq na kusema kuwa, aliwahi kwenda mara mbili nchini Saudi Arabia kwa ajili ya kuonana na watu wakubwa na kukusanya fedha za kuendeshea genge hilo.

Kwa mujibu wa mtandao wa habari wa al Ahd, mufti huyo wa Daesh amefichua hayo katika mahojiano maalumu na kusema kuwa, misimamo yake mikali ilianza tangu mwaka 2003. Mwaka huo alielekea katika nchi moja jirani kwa ajili ya masomo ya dini na alitiwa mbaroni na utawala wa zamani wa Iraq mwaka 1997 kutokana na kujiunga kwake na magenge yenye misimamo mikali.

Mufti wa genge la kigaidi la Daesh

 

Mufti huyo wa genge la kigaidi la Daesh ameongeza kuwa, mwaka 2006 makundi yenye silaha yalishuhudia mabadiliko makubwa. Nilikwenda mjini Makkah, Saudi Arabia kuonana na Ayoub Mustafa al Iraqi aliyekuwa na uraia wa nchi moja ya Ulaya. Alinitaka nimpe maelezo ya kutosha kuhusu makundi yenye silaha ya Kisunni nchini Iraq, tab'an nami nilipewa fedha nyingi za kuanzisha kituo maalumu cha kuhifadhisha Qur'ani kama chaka kwani lengo hasa lilikuwa ni kuyasaidia kifedha makundi ya wabeba silaha. 

Amma kuhusu safari yake ya pili ya kuitembelea Saudia, mufti huyo wa genge la kigaidi la Daesh anasema, mara hiyo alikwenda kuonana na mufti mmoja Msaudia kumuomba ayasaidie kifedha makundi yenye silaha nchini Iraq na yeye hakusita kufanya hivyo. Mufti huyo wa Daesh alihusika pia na kuripua sehemu aliyekuwa amezikwa Nabii Yunus AS na baadaye alifanya makusudi kupotosha suala hilo.