Chuki za viongozi wa Saudia kwa Ikhwanul Muslimin, zazidi kuwa kubwa
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i65028-chuki_za_viongozi_wa_saudia_kwa_ikhwanul_muslimin_zazidi_kuwa_kubwa
Duru za kuaminika zimetangaza habari ya kuongezeka sana chuki za viongozi wa Saudi Arabia dhidi ya chama cha al Islah, tawi la kundi la Ikhwanul Muslimin, licha ya kwamba pande hizo mbili zimekuwa zikishirikiana kwa miaka mingi sasa katika vita dhidi ya wananchi wa Yemen.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 05, 2020 21:14 UTC
  • Chuki za viongozi wa Saudia kwa Ikhwanul Muslimin, zazidi kuwa kubwa

Duru za kuaminika zimetangaza habari ya kuongezeka sana chuki za viongozi wa Saudi Arabia dhidi ya chama cha al Islah, tawi la kundi la Ikhwanul Muslimin, licha ya kwamba pande hizo mbili zimekuwa zikishirikiana kwa miaka mingi sasa katika vita dhidi ya wananchi wa Yemen.

Mtandao wa "26 Septemba" umezinukuu duru za kuaminika za Yemen zikisema kuwa, viongozi wa chama cha al Islah, tawi la kundi la Ikhwanul Muslimin katika kipindi cha wiki mbili zilizopita wamekuwa wakipigania kuonana na Mohammad bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia ili kumthibitishia kuwa hawana uhusiano wowote na Ikhwanul Muslimim, lakini Bin Salman amekataa kuonana nao.

Viongozi wa chama cha al Islah hawakutosheka na hapo katika kuwabembeleza viongozi wa Saudi Arabia, bali wamewatumia pia ujumbe mbalimbali wakitangaza kuwa hawana uhusiano na kundi la Ikhwanul Muslimin, lakini haikusaidia kitu kwa sababu baadhi ya mamluki wa Saudia nchini Yemen wameipa Riyadh ushahidi uonaoonesha kuwa viongozi wa chama cha al Islah cha Yemen bado wana uhusiano na Ikhwanul Muslimin.

Chama cha al Islah cha Yemen, tawi la kundi la Ikhwanul Muslimin

 

Sasa hivi kumezuka mzozo mkubwa ndani ya chama cha al Islah ambacho tawi lake la kijeshi ni rafiki mkubwa wa Saudi Arabia tangu ukoo wa Aal Saud ulipoanzisha uvamizi wa pande zote dhidi ya wananchi wa Yemen kwa kushirikiana na ukoo wa Aal Nahyan wa Imarati, baadhi ya tawala vibaraka za Kiarabu kama Sudan na mamluki kutoka ndani na nje ya Yemen. 

Uvamizi wa Saudia huko Yemen ambao ulianza mwaka 2015, una baraka kamili na unasaidiwa kwa kila hali na madola ya kibeberu kama Marekani, utawala wa Kizayuni na nchi za Magharibi. Mamilioni ya wananchi Waislamu wa Yemen wanateseka hadi hivi sasa kutokana na uvamizi huo.