Answarullah: Wavamizi hawatokuwa salama madhali Wayemen hawana usalama
Mmoja wa viongozi waandamizi wa Ofisi ya Kisiasa ya Aswarullah ya Yemen amesisitiza kuwa, nchi zilizoivamia hiyo hiyo kamwe haziwezi kuwa salama maadamu zinaendelea kuwakosesha usalama wananchi wa Yemen.
Shirika la habari la IRIB leo Jumanne limenukuu Bw. Muhammad al Bukhaiti akisema hayo na kuongeza kuwa, kukomeshwa uvamizi nchini Yemen, kundolewa vikwazo, kuacha wavamizi kuizingira nchi hiyo na kupatikana amani katika eneo ni kwa manufaa ya nchi zote hata zilizoivamia Yemen.
Al Bukhaiti amelaani kuendelea mashambulizi ya muungano vamizi wa Yemen unaoongozwa na Saudi Arabia na kusema kuwa, serikali ya nchi hiyo kamwe haiwezi kuitia hatarini hadhi na heshima ya nchi hiyo kupitia kujisalimisha kwa maadui.
Mwezi Machi 2015, Saudi Arabia kwa uungaji mkono wa Marekani, Utawala wa Kizayuni wa Israel, Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na waitifaki wao wengine, ilianzisha uvamizi wa pande zote wa kijeshi dhidi ya wananchi maskini wa nchi ya Kiarabu ya Yemen. Tangu wakati huo hadi hivi sasa, wavamizi hao wameizingira kila upande nchi hiyo ya Waislamu, kutokea angani, ardhini na baharini.
Saudia na wavamizi wenzake walianzisha vita hivyo vya pande zote dhidi ya Yemen mwaka 2015 kwa tamaa kuwa wangeliweza kumaliza vita hivyo haraka sana na kulisambaratisha jeshi na vikosi vya kujitolea vya wananchi. Hata hivyo ndoto yao hiyo imeshindwa kuaguka.
Mashambulizi ya kikatili na ya pande zote ya Saudi Arabia na wenzake yameshapelekea zaidi ya watu 16 elfu kuuawa nchini Yemen, makumi ya maelfu ya wengine kujeruhiwa na mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi.