Mshauri wa Assad ataka jeshi vamizi la Marekani liondoke Syria
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i65297-mshauri_wa_assad_ataka_jeshi_vamizi_la_marekani_liondoke_syria
Mshauri wa Rais Bashar al Assad wa Syria amelaani vikali Marekani kwa kuikalia kwa mabavu nchi yake na kupora utajiri wake wa mafuta.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 20, 2020 03:41 UTC
  • Mshauri wa Assad ataka jeshi vamizi la Marekani liondoke Syria

Mshauri wa Rais Bashar al Assad wa Syria amelaani vikali Marekani kwa kuikalia kwa mabavu nchi yake na kupora utajiri wake wa mafuta.

Katika mahojiano na Televisheni ya al-Mayadeen, Bouthaina Shaaban, mshauri wa Rais Assad katika masuala ya vyombo vya habari amesisitiza kuwa ni lazima Marekani iondoe askari wake vamizi nchini Syria.

Amesema Damascus inasubiri kuona rais ajaye wa Marekani, Joe Biden, atachukua muelekeo upi kuhusu Syria lakini amesisitiza kuwa nukta muhimu zaidi ni kuondoka askari wa Marekani nchini Syria.

Amesema Wasyria hawatarajii mengi kutoka kwa rais mpya wa Marekani kwani  eneo la Asia Magharibi limekuwa likipata masaibu mikononi mwa tawala zote za Warepublican na Wademocrat.

Shaaban aidha amemtaka Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Kelly Craft atambue azimio nambari 2254 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo linapinga vikosi vya Marekani kukalia kwa mabavu ardhi ya Syria.

Tokea mwaka 2011, Jeshi la Syria limekuwa likipambana na magaidi wanaopata himaya ya kigeni. Wanajeshi wa Syria wakiwa wanapata uungaji mkono wa Jeshi la Anga la Russia na washauri wa kijeshi wa Iran wamefanikiwa kudhibiti karibu maeneo yote ya nchi hiyo ambayo yalikuwa yametekwa na magaidi wakufurishaji.

Magaidi wa ISIS wanaopata himaya ya Marekani

Katika upande wa pili Marekani imekuwa ikiwaunga mkono magaidi ambao wanataka kuiangusha serikali ya Rais Assad sambamba na kupora mafuta ghafi ya petrol ya Syria.

Wiki iliyopita, shirika rasmi la habari la Syria SANA liliripoti kuwa msafara wa jeshi la Marekani wa magari na malori 85 ya mafuta ulivuka kivuko kilichopigwa marufuku cha Al Walid karibu na eneo la At-Tanaf na kuingia mkoa wa Al Anbar nchini Iraq.

Malori 16 ya deraya yalikuwa yakiusindikiza msafara huo wa jeshi la kigaidi na kiharamia la Marekani.

Katika miezi ya Oktoba na Novemba pia askari wa jeshi la kigaidi la Marekani walipora katika awamu mbili malori 107 ya mafuta ya Syria na kuyasafirisha kimagendo kuyapeleka Iraq kupitia kituo cha mpakani cha Hamzah Beik kilichoko kwenye mpaka wa pamoja wa nchi hizo mbili. Matukio ya aina hiyo yameripotiwa mara kadhaa katika kipindi cha miaka na miezi ya karibuni.