Hamas yaikosoa Imarati kwa kuunga mkono sera za Israel
Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema kuwa, Umoja wa Falme za Kiarabu unaunga mkono sera za utawala wa Kizayuni wa Israel kwa madhara na ukiukaji wa haki za Wapalestina.
Sami Abu Zuhri amesema hayo katika ujumbe wake wa Twitter na kuongeza kuwa: Matamshi yaliyotolewa na baadhi ya maafisa wa Imarati walipoitembelea Israel yalivuka mstari na kufichua uungaji mkono usio na mipaka wa UAE kwa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni na kukaliwa kwa mabavu ardhi za Wapalestina.
Amesema kauli za namna hiyo zinaonesha namna Umoja wa Falme za Kiarabu unavyoshirikiana na utawala ghasibu wa Israel katika kukanyaga haki za wananchi wa Palestina na maslahi ya watu wa eneo hili la Asia Magharibi.
Katika ziara za hivi karibuni huko Israel na katika Miinuko ya Golan ya Syria inayokaliwa kwa mabavu na Wazayuni maghasibu, maafisa wa Imarati na Bahrain walitoa matamshi yanayoonesha uungaji mkono wao kwa sera ghalati za Tel Aviv.
Kabla ya hapo, Izzat al-Rishq, mjumbe mwadamizi wa Idara ya Kisiasa ya HAMAS alisema kuwa, hatua ya baadhi ya mataifa ya Kiarabu ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel ni kumhudumia adui Mzayuni.
Itakumbukwa kuwa, tarehe 25 Septemba, Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Imarati na Bahrain walisaini mkataba wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel katika hafla iliyofanyika katika Ikulu ya White House mjini Washington, Marekani.