Haniya: Kuanzisha uhusiano na Israel ni kuupiga jambia umma wa Kiislamu
(last modified Thu, 24 Dec 2020 08:04:11 GMT )
Dec 24, 2020 08:04 UTC
  • Haniya: Kuanzisha uhusiano na Israel ni kuupiga jambia umma wa Kiislamu

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema kitendo cha baadhi ya nchi za Kiarabu cha kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel ni sawa na kuwapiga jambia kwa nyuma wananchi wa Palestina na umma wa Kiislamu kwa ujumla.

Ismail Haniya amesema hayo katika ujumbe aliowaandikia zaidi ya viongozi 30 wa nchi za Kiislamu na Kiarabu na kusisitiza kuwa, kufanya wa kawaida uhusiano na utawala huo haramu ni kosa kubwa la kistratejia.

Amesema hatua hiyo ya baadhi ya nchi za Kiarabu ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel itakuwa na taathira hasi kwa maslahi ya umma wa Kiislamu na ni hatari kubwa kwa kadhia ya Palestina.

Haniya ameeleza bayana kuwa, suala la Palestina hivi sasa lipo katika hatari kubwa na linakabiliwa na changamoto tele kutokana na usaliti huo wa baadhi ya watawala wa Kiarabu wa kukubali kurubuniwa na kushinikizwa kuanzisha uhusiano na Tel Aviv.

Maandamano ya kupinga uhusiano na Israel nchini Tunisia

Hivi karibuni mfalme wa Morocco Mohammed VI alimwarifu Rais Donald Trump wa Marekani kwenye mazungumzo kwa njia ya simu kuwa amekubali kurejesha mawasiliano ya kiserikali na kuanzisha uhusiano wa kibalozi na utawala wa Israel haraka iwezekanavyo.

Itakumbukwa kuwa, tarehe 25 Septemba, Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Imarati na Bahrain walisaini mkataba wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel katika hafla iliyofanyika Ikulu ya White House mjini Washington.

Sudan pia imefuata mkumbo huo huo na kutangaza utayarifu wa kuanzisha uhusiano na utawala huo bandia unaoua na kuwadhulumu wananchi wa Paletina kila leo.

Tags