Marekani yawaingiza magaidi katika kituo chake cha kijeshi Syria
Jeshi la Marekani limewaingiza makumi ya magaidi wa ISIS au Daesh katika kituo chake cha kijeshi cha Al Tanf ambacho kiko Syria kinyume cha sheria.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Syria (SANA), siku ya Jumanne, magari ya deraya ya Jeshi la Marekani yalishiriki katika oparesheni ya kuwaachilia huru makumi ya magaidi wa ISIS waliokuwa katika jela ya Kamb al Bulgar mashariki mwa mji wa Al Shadadi katika mkoa wa Al Hasakah kaskazini mashariki mwa Syria na kuwapeleka katika kituo chao kijeshi cha Marekani cha Al Tanf katika mkoa wa Homs.
Kwa mujibu wa taarifa, Marekani imewahamisha baadhi ya magaidi hao wa ISIS kutoka al-Hasakah hadi la Tanf kwa helikopta.
Jeshi la Marekani na wanamgambo wa Kikurdi wa SDF wenye mfungamano na Marekani wako kinyume cha sheria kaskazini na kaskazini mashariki mwa Syria ambapo mbali na kupora utajiri wa mafuta wa eneo hilo wanatekeleza hujuma dhidi ya Jeshi la Syria na Wasyria katika eneo hilo.
Majeshi ya Marekani yanatumia magaidi wa ISIS kutekeleza njama zao chafu za kuibua machafuko na vita katika eneo la Asia Magharibi.