UN yaikosoa Marekani kwa kukwamisha mchakato wa kurejesha amani Yemen
-
Stéphane Dujarric
Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amekosoa uamuzi wa Marekani wa kuiweka harakati ya Ansarullah ya Yemen katika orodha ya makundi ya kigaidi na kusema kuwa ni pigo kwa mchakato wa kisiasa wa nchi hiyo.
Stéphane Dujarric amekosoa uamuzi wa Ikulu ya Rais wa Marekani, White House dhidi ya Yemen na ameitaka Washington iruhusu kupelekwa misaada ya kibinadamu kwa raia wote wa Yemen haraka iwezekanavyo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo Jumatatu ya jana alitangaza kuwa wizara hiyo ina nia ya kuliwasilisha jina la harakati ya Ansarullah katika Kongresi kama kundi la kigaidi. Wakati huo huo Marekani imepanga kuyaweka majina ya viongozi wa harakati hiyo ya wananchi wa Yemen katika orodha ya magaidi wa kimataifa.
Uamuzi huo umepingwa pakubwa na duru mbalimbali na umetajwa na wataalamu wa mambo kuwa ni harakati hasi na haribifu hususan kwa kutilia maanani hali ya sasa ya Yemen.
Saudi Arabia, Marekani, Imarati na washirika wao walianzisha vita dhidi ya Yemen mwaka 2015 na kuizingira nchi hiyo kutoka pande zote. Hata hivyo Saudia ya washirika wake wameshindwa kufikia malengo yao kutokana na mapambano ya mashujaa wa taifa la Yemen.