Jihadul Islami: Shahidi Soleimani ameimarisha makundi ya Palestina
Mwakilishi wa harakati ya Jihadul Islami ya Palestina hapa Tehran amepongeza nafasi ya Luteni Jenerali Shahidi Qassem Soleimani na kusema: Shahidi Soleimani aliyaunganisha na kuyaimarisha makundi ya muqawama ya Palestina mbele ya utawala wa Kizayuni.
Akizungumza leo Jumanne hapa Tehran katika mahojiano na shirika la habari la Iran Press, Nasser Abu Sharif ameeleza kuwa: Shahidi Soleimani aliunga mkono muqawama na mapambano dhidi ya mabeberu na akasema: Muqawama usingeweza kukabiliana na kusimama kidete mbele ya mashambulizi hatari ya Wazayuni na Marekani kama isingekuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Haj Qassem Soleimani, wanajihadi wenzake na uungaji wao mkono usio na ukomo.
Abu Sharif ameongeza kuwa: Shahidi Soleimani alikuwa na nafasi kuu katika kuunganisha na kuimarisha ari ya mhimili wa muqawama; na hilo ndilo lililoimarisha nguvu ya mhimili wa muqawama mkabala wa utawala Kizayuni na njama za Magharibi.
Mwakilishi wa harakati ya Jihadul Islami ya Palestina hapa Tehran amezungumzia pia mazoezi ya karibuni ya makundi ya muqawama ya Palestina huko Ghaza na ujumbe wake na kueleza kuwa: Maneva hayo ya karibuni yaliyofanyika sambamba na kumbukumbu ya kutimia mwaka mmoja tangu kuuliwa kigaidi Haj Qassem Soleimani yamedhihirisha umoja uliopo baina ya makundi ya muqawama mkabala na utawala wa Kizayuni. Luteni Jenerali Qassem Soleimani aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (Sepah) aliuawa shahidi tarehe Tatu Januari mwaka jana 2020 katika shambulio la anga la wanajeshi vamizi na magaidi wa Marekani karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad, Iraq.