Abdullah: Taliban inakazania kuendeleza vita Afghanistan
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i66028-abdullah_taliban_inakazania_kuendeleza_vita_afghanistan
Mkuu wa Baraza Kuu la Maslahi ya Taifa la Afghanistan amesema, hatua ya Taliban ya kupanua wigo wa machafuko na vitendo vya utumiaji nguvu inaonyesha kuwa kundi hilo linakazania na kushupalia kuendeleza vita nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 24, 2021 01:09 UTC
  • Abdullah: Taliban inakazania kuendeleza vita Afghanistan

Mkuu wa Baraza Kuu la Maslahi ya Taifa la Afghanistan amesema, hatua ya Taliban ya kupanua wigo wa machafuko na vitendo vya utumiaji nguvu inaonyesha kuwa kundi hilo linakazania na kushupalia kuendeleza vita nchini humo.

Abdullah Abdullah ameyasema hayo katika hafla iliyofanyika mji mkuu wa Afghanistan, Kabul na kuongeza kuwa, wananchi wa Afghanistan walikuwa na mategemeo kwamba katika duru ya pili ya mazungumzo ya amani, wawakilishi wa serikali na wa Taliban wataweza angalau kufikia makubaliano ya kupunguza machafuko, lakini jambo hilo bado halijawezekana; na sababu yake ni msimamo wa Taliban wa kushupalia na kukazania kuendeleza vita.

Mkuu wa Baraza Kuu la Maslahi ya Taifa la Afghanistan ametoa matamshi hayo katika hali ambayo, baada ya kupita takriban siku ishirini tangu ilipoanza duru ya pili ya mazungumzo ya amani ya Afghanistan katika mji mkuu wa Qatar, Doha si tu mazungumzo hayo hayajapiga hatua, lakini inasemekana kuwa yameshaingia kwenye mkwamo mwingine mpya.

Wawakilishi wa Taliban katika mazungumzo ya amani ya Afghanistan

Wakati huohuo Rais Ashraf Ghani wa Afghanistan amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na mawaziri wakuu wa Australia, Canada na Norway na kutilia mkazo kutekelezwa usitishaji vita nchini Afghanistan.

Kupunguzwa machafuko na kusitishwa mapigano ndicho kipaumbele cha ujumbe wa serikali ya Afghanistan katika mazungumzo ya amani ya Doha, lakini kundi la Taliban linasisitiza kujadiliwa kwanza namna utakavyokuwa mfumo ujao wa kisiasa wa Afghanistan.../