Wazayuni wamevunja zaidi ya nyumba nyingine 800 za Wapalestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i66118-wazayuni_wamevunja_zaidi_ya_nyumba_nyingine_800_za_wapalestina
Mwaka 2020, utawala wa Kizayuni wa Israel ulivunja nyumba 869 za Wapalestina na taasisi nyingine mbalimbali za wananchi hao wanaodhulumiwa kila upande.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 26, 2021 03:57 UTC
  • Wazayuni wamevunja zaidi ya nyumba nyingine 800 za Wapalestina

Mwaka 2020, utawala wa Kizayuni wa Israel ulivunja nyumba 869 za Wapalestina na taasisi nyingine mbalimbali za wananchi hao wanaodhulumiwa kila upande.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRIB, mwaka uliopita wa 2020, wanajeshi makatili wa Israel walivunja nyumba na taasisi 869 za Wapalestina na wakang'oa miti 6,507 ya matunda katika mashamba ya Wapalestina huko katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan pekee.

Miji ya Wapalestina iliyokumbwa zaidi na jinai ya kuvunjwa nyumba za wananchi kunakofanywa na wanajeshi wa utawala dhalimu wa Israel, ni Baytul Muqaddas, al Khalil na Tubas.

Israel inatumia wanajeshi wake makatili kuvunja nyumba za Wapalestina

 

Jana Jumatatu, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) ilitangaza kuwa, katika kipindi cha wiki mbili zilipita, utawala wa Kizayuni umevunja nyumba 24 wa wananchi wa Palestina kwa madai ya uongo ya kutokuwa na kibali cha kujenga. Jinai hiyo imesababisha wananchi 34 wa Palestina wawe wakimbizi na kiujumla wananchi 70 wa Palestina wamepata hasara kutokana na dhulma hiyo ya Israel.

Jamie McGoldrick, mratibu wa masuala ya misaada ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa hivi karibuni alisema kuwa, katika miezi ya hivi karibuni na licha ya kuenea maambukizi ya kirusi hatari cha corona, utawala wa Kizayuni wa Israel umeendelea kuvunja nyumba za Wapalestina kinyume cha sheria na kuwafanya wakimbizi wakazi wake.

Tarehe 23 Disemba 2016, Umoja wa Mataifa ulipasisha azimio nambari 2334 lililotoa amri kwa utawala wa Kizayuni wa Israel kuacha mara moja ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi unazowapora Wapalestina. Hata hivyo Marekani inakwamisha utekelezaji wa azimio hilo.