Harakati ya Ansarullah yataka Umoja wa Mataifa ujadili maafa ya Yemen
Harakati ya Ansarullah ya Yemen imetoa wito kwa wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wajadili hali mbaya ya kibinaadamu nchini Yemen ambayo imetokana na uvamizi wa muungano unaoongozwa na Saudia.
Mohammad Ali Al Houthi, mwanachama wa Baraza Kuu la Kisiasa la Harakati ya Ansarullah ya Yemen ameandika ujumbe katika ukurasa wake wa Twitter na kutoa wito kwa wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutembelea Yemen ili wajionee kwa karibu maafa yaliyosababishwa na uvamizi wa Saudia.
Aidha Mohammad Ali Al Houthi amesema hali nchini Yemen ni mbaya sana kiasi kuwa inaweza kutajwa kuwa ni 'maafa makubwa zaidi ya kibinadamu duniani'.
Hayo yanajiri katika hali ambayo Jumuiya ya Kutetea Hali za Wanawake na Watoto ya Yemen imetangaza kuwa, watoto na wanawake wapatao 13,088 wameuawa shahidi au kujeruhiwa katika hujuma ya muungano vamizi wa Saudia nchini humo.
Hivi karibuni, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) lilisema kati ya Januari na Juni 2021, asilimia 54 ya Wayemen, yaani watu milioni 16.2, watakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula.
Aidha mwezi Disemba mwaka jana, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) ilitangaza kuwa vita vya Saudi Arabia dhidi ya Yemen vimepelekea zaidi ya watu 233,000 kupoteza maisha katika kipindi cha miaka sita iliyopita.
Ikumbukwe kuwa mnamo mwezi Machi 2015 Saudi Arabia, ikiungwa mkono na Marekani, utawala haramu wa Israel, Umoja wa Falme za Kiarabu na nchi zingine kadhaa iliivamia kijeshi Yemen na kuiwekea mzingiro wa kila upande.
Utawala dhalimu wa Saudia ulianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen kwa lengo la kuiondoa madarakani Harakati ya Ansarullah na kumrejesha madarakani kibaraka wake, Abdrabbuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kukimbilia Riyadh. Hata hivyo hadi sasa Saudia na washirika wake wameshindwa kufikia malengo yao kutokana na kusimama kidete wananchi wa Yemen.