Wapalestina watungua ndege ya kijasusi ya Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i66342-wapalestina_watungua_ndege_ya_kijasusi_ya_israel
Wanamapambano wa Kiislamu wa Palestina, usiku wa kuamkia leo wametungua ndege moja isiyo na rubani ya utawala wa Kizayuni iliyokuwa ikifanya ujasusi katika anga ya Ukanda wa Ghaza.
(last modified 2026-05-20T03:07:53+00:00 )
Feb 01, 2021 04:49 UTC
  • Wapalestina watungua ndege ya kijasusi ya Israel

Wanamapambano wa Kiislamu wa Palestina, usiku wa kuamkia leo wametungua ndege moja isiyo na rubani ya utawala wa Kizayuni iliyokuwa ikifanya ujasusi katika anga ya Ukanda wa Ghaza.

Shirika la habari la Tasnim limezinukuu duru za Palestina zikitangaza habari hyo na kusema kuwa, droni hiyo ya Israel sasa hivi iko mikononi mwa wanamapambano wa Kiislamu wa Palestina.

Duru hizo zimeongeza kuwa, ndege hiyo isiyo na rubani ya utawala wa Kizayuni imetunguliwa katika eneo la Bait Hanun, kaskazini mwa Ukanda wa Ghaza.

Katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni, ndege zisizo na rubani, ndege za kijeshi, helikopta na mizinga ya utawala wa Kizayuni imekuwa ikitumika kufanya mashambulizi katika maeneo mbalimbali ya Ukanda wa Ghaza.

Bendera ya utawala wa Kizayuni wa Israel

 

Tangu mwezi Disemba 2017 hadi hivi sasa utawala wa Kizayuni wa Israel umeanzisha wimbi jipya la mashambulio ya mara kwa mara ya kikatili dhidi ya Wapalestina wasio na ulinzi wa Ukanda wa Ghaza.

Hadi hivi sasa maelfu ya Wapalestina wameshauawa shahidi na kujeruhiwa katika mashambulizi hayo ya kidhalimu ya Israel.

Hii ni katika hali ambayo tangu mwaka 2006 hadi hivi sasa utawala wa Kizayuni wa Israel umewafungia njia zote wananchi wa Ghaza kiasi kwamba watu hawawezi kuingia wala kutoka katika eneo hilo. Sasa hivi Ukanda wa Ghaza unahesabiwa kuwa ni jela kubwa ya ardhini duniani kutokana na Israel kutoruhusu chochote kuingia wala kutoka katika eneo hilo.

Kosa la Wapalestina kwa mtazamo wa mabeberu wa dunia wakiwemo Wazayuni, ni kutumia haki yao ya kidemokrasia ya kuichagua Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina kuwaongoza katika uchaguzi uliotimiza masharti yote wa mwaka 2006.