Wazayuni wamezuia adhana mara kadhaa katika Msikiti wa Nabii Ibrahim AS
Wakuu wa Utawala wa Kizayuni wa Israel wanazuia adhana kuadhiniwa katika Msikiti wa Nabii Ibrahim, Amani iwe juu yake, ulioko katika mji wa Al Khalil au Hebron huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Palestina, wakuu wa utawala dhalimu wa Israel wanatumia kila mbinu kujaribu kuufunga, kuuhujumu na kuuharibu msikiti huo mbali na kuzuia kusomwa adhana hapo mara kwa mara.
Kwa mujibu wa ripoti ya Wizara ya Wakfu na Masuala ya Kidini ya Palestina, katika mwezi uliopita wa Januari pekee, Wazayuni walizuia adhana kuadhiniwa mara 50 katika Msikiti wa Nabii Ibarahim AS.
Wazayuni wanazuia adhana, hasa adhana ya Magharibi, katika msikiti huo mtakatifu kwa kisingizo cha kuwa sauti ya adhana inawakera walowezi wa Kizayuni katika eneo hilo.
Njama nyingine inayotekelezwa na Wazayuni ili hatimaye waweze kutimiza ndoto yao chafu ya kuutwaa msikiti huo ni kuzuia kamati ya ukarabati wa msikiti huo kutekeleza shughuli zake.
Msikiti wa Ibrahim AS uko katika kitongoji cha kale cha Al Khalil (Hebron) kusini mwa Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Kwa mujibu wa baadhi ya Hadithi, ndani ya msikiti huo kuna kaburi la Nabii Ibrahim AS na mkewe Sarah na vile vile makaburi ya Manabii Is-haq na Yaaqub AS na ya wake zao.