Misafara 2 ya kijeshi ya Marekani yashambuliwa nchini Iraq
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i66478-misafara_2_ya_kijeshi_ya_marekani_yashambuliwa_nchini_iraq
Duru za kiusalama zimeripoti habari ya kushambuliwa misafara miwili ya kilojistiki ya jeshi vamizi la Marekani katikati na kusini mwa Iraq.
(last modified 2026-02-11T16:16:55+00:00 )
Feb 05, 2021 02:51 UTC
  • Misafara 2 ya kijeshi ya Marekani yashambuliwa nchini Iraq

Duru za kiusalama zimeripoti habari ya kushambuliwa misafara miwili ya kilojistiki ya jeshi vamizi la Marekani katikati na kusini mwa Iraq.

Inaarifiwa kuwa, msafara wa kwanza wa jeshi la Marekani ulishambuliwa katika mkoa wa Babil katikati mwa Iraq huku wa pili ukihujumiwa katika mkoa wa Basra ulioko kusini mwa nchi hiyo ya Kiarabu.

Kundi la Qasim al-Jabbarin limetangaza kuhusika na shambulizi la mkoa wa Babil, huku kundi la Saraya Awliya al-Dam likikiri kuhusika na shambulizi la pili katika mkoa wa Basra.

Haijabainika iwapo mashambulizi hayo ya jana Alkhamisi yamesababisha maafa mbali na kulitia hasara jeshi vamizi la Marekani lililoko Iraq.

Katika miezi ya hivi karibuni, misafara ya kilojistiki ya jeshi la Marekani imekuwa ikishambuliwa mara kwa mara katika hujuma za mabomu ya kutegwa kando kando ya barabara za Iraq.

Upinzani dhidi ya uwepo wa askari vamizi wa Marekani nchini Iraq ulishtadi tokea Januari mwaka jana, baada ya jeshi la kigaidi la US kuwaua kikatili aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), Luteni Jenerali Qassem Soleimani na Naibu Kamanda wa harakati ya wananchi wa Iraq ya Hashdu Shaabi, Abu Mahdi al-Muhandis katika mji mkuu Baghdad.

Baada ya jinai hiyo, Bunge la Iraq mnamo Januari 5 mwaka uliopita 2020 lilipasisha muswada wa sheria ya kutaka kuondoka nchini humo majeshi yote ya kigeni.