Ansarullah: Wayemen hawahadaiki kwa maneno ya Biden
Mjumbe wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen na msemaji wa harakati ya Ansarullah wamesema kuhusu madai ya Marekani ya kusitisha uungaji mkono wake kwa vita dhidi ya nchi hiyo kwamba, Wayemen hawahadaiki kwa maneno hayo.
Muhammad Ali al-Houthi, mjumbe wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen ametoa jibu kwa madai hayo kupitia ujumbe aliotuma kwenye ukurasa wa Twitter akisisitiza kuwa, hatua yoyote ambayo haitahitimisha mzingiro dhidi ya Yemen haitazingatiwa wala kupewa umuhimu wowote.
Jack Sullivan, mshauri wa usalama wa taifa katika Ikulu ya White House alisema jana kuwa, rais Joe Biden wa Marekani atasimamisha uungaji mkono wa nchi yake kwa operesheni za hujuma za kijeshi dhidi ya Yemen.
Naye Muhammad Abdusalam, mkuu wa timu ya mazungumzo ya serikali ya uokovu wa kitaifa ya Yemen na ambaye pia ni msemaji wa harakati ya Ansarullah amesisitiza kuwa, kurejeshwa amani nchini Yemen kunategemea na kuhitimishwa uvamizi na mzingiro dhidi ya nchi hiyo.
Abdusalam amebainisha kuwa, chaguo la uvamizi na mzingiro la muungano unaoongozwa na Saudia limewasababishia wavamizi hao kipigo kikali cha muqawama wa kupigiwa mfano cha taifa kubwa la Yemen.
Msemaji huyo wa harakati ya Ansarullah ameashiria uwezo wa kuzuia hujuma wa makombora ya nchi yake dhidi ya muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia na akabainisha kwamba, makombora ya Yemen yapo kwa ajili ya kuilinda nchi; na kusitishwa kwake kunategemea na kusimamishwa kikamilifu uchokozi na mzingiro.
Kwa msaada na uungaji mkono wa Marekani, Imarati na nchi zingine kadhaa, mwezi Machi 2015 Saudi Arabia ilianzisha uvamizi wa kijeshi dhidi ya Yemen na kuiwekea mzingiro nchi hiyo wa nchi kavu, baharini na angani. Moto wa vita uliowashwa na Saudia na washirika wake, hadi sasa umeshateketeza roho za watu zaidi ya 16,000 nchini Yemen, mbali na kujeruhi makumi ya maelfu pamoja na kusababisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi.../