Imarati, Bahrain zawakatia Wapalestina misaada baada ya kuikumbatia Israel
Umoja wa Falme za Kiarabu na Bahrain zimepunguza kwa kiasi kikubwa misaada yao ya kifedha iliyokuwa ikiwapa wananchi wa Palestina, baada ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Hayo yameripotiwa na kanali ya 12 ya televisheni ya Kizayuni ambayo imedai kuwa, katika hali ambayo Imarati ililipa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNRWA) misaada ya dola milioni 53 na 51 mwaka 2018 na 2019 kwa usanjari huo, lakini mwaka jana ililipa tu dola milioni moja.
Aidha ripoti hiyo imeeleza kuwa Bahrain imewapunguzia pia Wapalestina misaada yao ya kifedha, ingawaje haijaainisha kiwango cha fedha kilichopunguzwa.
Ikumbukwe kuwa, Agosti 31 mwaka 2018, serikali iliyopita ya Marekani ya Donald Trump ilikata misaada yote ya kifedha kwa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNRWA), huku ikipuuza matatizo ya kifedha ya shirika hilo.
Lengo la utawala wa Trump limejikita zaidi katika njama za kuhakikisha kwamba, misaada ya kifedha ya nchi nyingine kwa asasi hiyo inayofanya shughuli zake chini ya Umoja wa Mataifa nayo inakatwa na kusimamishwa.
Katika miezi mitatu ya mwisho wa mwaka uliomalizika wa 2020, nchi nne za Kiarabu za Imarati, Bahrain, Sudan na Morocco zilianzisha uhusiano rasmi na utawala haramu wa Kizayuni na Israel. Hatua hiyo ya kihaini na ya usaliti iliyofanywa na nchi hizo ambayo ni kushiriki kwenye mpango wa mapatano wa Kimarekani na Kizayuni, imelaaniwa na kukosolewa vikali katika Ulimwengu wa Kiislamu.