Makundi 14 ya Palestina yaelekea Cairo kushiriki katika mazungumzo ya kitaifa
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i66590-makundi_14_ya_palestina_yaelekea_cairo_kushiriki_katika_mazungumzo_ya_kitaifa
Duru za habari zimearifu kuwa jumbe za makundi 14 ya Palestina zimeelekea Cairo nchini Misri kushiriki katika vikao vya mazungumzo ya kitaifa ya Palestina.
(last modified 2026-08-17T09:53:57+00:00 )
Feb 07, 2021 23:14 UTC
  • Makundi 14 ya Palestina yaelekea Cairo kushiriki katika mazungumzo ya kitaifa

Duru za habari zimearifu kuwa jumbe za makundi 14 ya Palestina zimeelekea Cairo nchini Misri kushiriki katika vikao vya mazungumzo ya kitaifa ya Palestina.

Mazungumzo ya kitaifa kati ya makundi ya Kipalestina kwa lengo la kuchunguza mafaili mawili makuu kuhusu mapatano ya kitaifa na namna ya kusimamia uchaguzi mkuu yanaanza leo Jumatatu huko Cairo mji mkuu wa Misri. 

Saleh al Aruri Naibu Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) ndiye Mwenyekiti wa ujumbe wa harakati hiyo katika mazungumzo hayo ya Cairo huku Harakati ya Fat-h ikiongozwa na Jibril Rajoub, Katibu wa Kamati Kuu ya harakati hiyo. 

Saleh al Aruri,Mkuu wa ujumbe wa Hamas katika mazungumzo ya Cairo 

Wakati huo huo Riyadh al Maliki Waziri wa Mambo ya Nje wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amekitaja kikao cha leo Jumatatu cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za Kiarabu huko Cairo kuwa chenye umuhimu mkubwa na kueleza kuwa kikao hicho kinafanyika kwa lengo la kuunga mkono malengo ya Palestina. 

Al Maliki amesisitiza kuwa: Ujumbe wa wazi kwa nchi zote duniani ikiwemo Marekani ni kwamba baadhi ya nchi za Kiarabu zinaheshimu mpango wa amani wa Waarabu na kuunga mkono malengo ya Palestina licha ya kuwepo mwenendo wa mapatano ya kisaliti ya baadhi ya nchi na utawala haramu wa Israel.

Shakhsiya wengine wengi binafsi pia wanashiriki katika mazungumzo hayo ya  leo Jumatatu  mjini Cairo,  mbali na makundi 14 ya Kipalestina.