Tishio la kurejea upya kundi la Daesh huko Iraq
Harakati za kundi la Daesh na pia mapigano kati ya kundi la Hashdu Shaabi la Iraq na masalia ya kundi hilo la kigaidi yameongezeka nchini humo katika miezi ya karibuni.
Kuna nukta kadha muhimu kuhusiana na jambo hilo.
Ya kwanza; chunguzi mbalimbali zinaonyesha kuwa harakati za masalia ya wananchama wa Daesh zimeongezeka zaidi katika mikoa ya Salahhudin na Diyala. Mkoa wa Diyala una mpaka wa pamoja na Iran, na ule wa Salahuddin pia hauko mbali sana na mipaka ya Iran. Wapo baadhi wanaoamini kwamba kundi la Daesh limeshadisisha hujuma kali huko Diyala na Salahuddin ili kutekeleza jambo kubwa zaidi. Wakati huo huo kuna uwezekano kwamba masalia hayo tajwa ya Daesh yameimarisha harakati zake katika maeneo mengine ya Iraq pia, harakati ambazo ni zaidi ya kutekeleza oparesheni za milipuko. Kuhusiana na kadhia hii tunaweza kuashiria kufanyiwa marekebisho muundo wa kundi la Daesh huko Iraq. Katika uwanja huo pia Harakati ya al Nujaba hivi karibuni ilitahadharisha juu ya kujitokeza upya kundi la Daesh huko Iraq.
Nukta ya pili; jeshi la Marekani limeingiza Iraq idadi kubwa ya magaidi kutoka Syria. Kuondoka huko Syria magaidi hao na kuingia Iraq ni moja ya sababu kuu za ukosefu wa amani unaoshuhudiwa sasa nchini humo. Katika mwaka mmoja wa karibuni, suala la kuondoka wanajeshi wa Marekani huko Iraq limejadiliwa pakubwa na kutiliwa maanani na baadhi ya makundi ya kisiasa na wananchi wa Iraq; na hivi sasa pia jambo hilo linaendelea kuchukuliwa kwa uzito mkubwa. Aidha mwishoni mwa utawala wa rais wa zamani wa Marekani Donald Trump, ilitangazwa kuwa wanajeshi kadhaa wa nchi hiyo wangeondoka huko Iraq. Inaonekana kuwa kuongezeka vitisho vya Daesh kuna mfungamano na suala la kuondoka wanajeshi wa Marekani; na nchi hiyo ya Magharibi pamoja na baadhi ya mirengo ya ndani ya Iraq inafanya jitihada za kutumia suala la kuongezeka vitisho vya Daesh ili wanajeshi wa Marekani waendelee kubaki katika nchi hiyo ya Kiarabu.
Nukta ya tatu; vikosi vya Hashdu Shaabi vimekuwa vikilengwa katika harakati za miezi ya hivi karibuni za masalia ya Daesh huko Iraq. Ni wazi kuwa, kundi la Daesh linaendesha mashambulizi ya moja kwa moja dhidi ya kundi la Hashdu Shaabi; ambalo tunaweza kulitaja kuwa ni kikosi cha usalama cha Iraq kilichojiimarisha na kujizatiti pakubwa ambacho kinaendelea kupkabiliana na mabaki ya magaidi wa Daesh na wakati huo huo kikipinga vikali kuendelea kusalia wanajeshi wa Marekani huko Iraq.
Aidha kundi la Hashdu Shaabi ni moja ya waitifaki wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huko Iraq. Kwa hivyo kutoa pigo kwa wapiganaji wa Hashdu Shaabi ni kati ya malengo muhimu ya hujuma za karibuni za kundi la Daesh huko Iraq.
Nukta ya nne; kubomolewa na kuharibiwa miundo mbinu ya Iraq pia ni moja ya malengo makuu ya harakati hizo tajwa za kundi la Daesh nchini humo. Kundi hilo adiha lilitoa pigo kubwa kwa miundombinu ya Iraq kuanzia mwaka 2014 hadi 2017. Hivi sasa pia wanachama wa Daesh wanafuatilia lengo hilo kwa sababu vitisho vyao vinapata nguvu kupitia kuharibu miundo mbinu na kuakisiwa pakubwa pia na vyombo vya habari; jambo ambalo lina umuhimu mkubwa kwa magaidi hao.
Na nukta ya tano na ya mwisho ni hii kuwa; kundi la Daesh limeibuka na kukulia katika mazingira ya kisiasa na kiusalama yenye kulegalega. Iraq ya sasa pia kwa upande mmoja inaongozwa na serikali ya muda, na katika upande mwingine kuna hitilafu na migawanyiko mikubwa kati ya makundi ya kisiasa nchini humo. Wakati huo huo kuna maelewano ya kiwango cha chini ndani ya Iraq kwa ajili ya kumuunga mkono Waziri Mkuu wa nchi hiyo Mustafa al Kadhimi. Katika upande wa pili, makundi ya kisiasa yanajishughulisha zaidi na uchaguzi ujao wa bunge; anga ambayo ni munasibu kwa kujihuisha upya Daesh. Ni kwa msingi huo ndipo baadhi ya makundi na shakhsia wa Iraq katika miezi ya karibuni wakatahadharisha mara kadhaa kuhusu hatari ya kuibuka upya Daesh nchini humo.