Abdulsalam: Martin Griffiths ni Muingereza katika joho la Umoja wa Mataifa
Msemaji wa harakati ya wananchi wa Yemen ya Ansarullah amesema kuwa mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika mgogoro wa Yemen, Martin Griffiths, ni Muingereza aliyevaa joho la Umoja wa Mataifa.
Muhammad Abdulsalam ameyasema hayo akijibu madai yaliyotolewa na Martin Griffiths akisema ana wasiwasi kutokana na kuanza tena hatua za kihasama huko mashariki mwa Yemen.
Abdulsalam amesema kuwa kama, ilivyo mantiki ya balozi wa Uingereza, Martin Griffiths pia ametaja hatua za taifa linaojitetea mbele ya hujuma za kigeni kuwa ni vitendo vya kihasama; anakariri madai ya mwakilishi wa Uingereza katika joho la Umoja wa Mataifa.
Msemaji wa harakati ya Ansarullah pia ameutuhumu Umoja wa Mataifa kuwa unasisitiza misimamo ya Marekani, Uingereza, Saudi Arabia na Imarati inayoendeleza mashaka na masaibu ya taifa la Yemen.
Muhammad Abdulsalam ambaye ndiye anayeongoza timu ya mazungumzo ya harakati ya Ansarullah ameongeza kuwa, mtu yeyote anayependa amani na suluhu anapaswa kutupilia mbali misimamo ya kundumakuwili.