Viashiria vya kuingia vita vya Yemen katika marhala mpya
Inaonekana kuwa vita vilivyoanzishwa na muungano vamizi huko Yemen chini ya uongozi wa Saudi Arabia vimengia katika marhala mpya.
Muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia ulianzisha vita huko Yemen tarehe 26 mwezi Machi mwaka 2015. Sababu kuu ya kuanzisha vita hivyo ni kutoridhishwa utawala wa Aal Saud na mchakato wa kuimarika Harakati ya Ansarullah katika muundo wa madaraka wa Yemen. Ni wazi kuwa, Harakati ya Ansarullah ilikusudia kuleta demokrasia ya kweli nchini humo kwa kuunga mkono matakwa ya wananchi, hata hivyo dhati na utambulisho wa utawala wa Saudia unapinga demokrasia na kuasisiwa utawala wa kiraia katika nchi hiyo. Kwa msingi huo, vita vilivyo kinyume cha sheria vikaanzishwa dhidi ya Yemen kwa lengo kuiweka kando na kuipindua Harakati ya wananchi ya Ansarullah huko Yemen. Mwezi ujao wa Miladia vita hivyo vitaingia katika mwaka wake wa saba.
Katika kukaribia kutimia mwaka wa sita tangu kuanzishwa vita hivyo; inaonekana kuwa vita hivyo tayari vimeingia katika marhala mpya kwa kuzingatia mchakato wa matukio yanayoendelea kujiri huko Yemen. Mapigano kati ya Saudi Arabia na Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen yangali yanaendelea. "Brigedia Jenerali Yahya Saree Msemaji wa jeshi la Yemen ametangaza kuwa kikosi cha anga cha nchi hiyo kimetungua ndege moja isiyo na rubani aina ya CH4 (droni) ya muungano vamizi wa Saudia iliyoundwa China. Droni hiyo ilikuwa ikifanya shughuli za kiuhasama katika anga ya Yemen huko mkoani Maarib ambapo ilitunguliwa kwa kombora la nchi kavu kwa anga. Hii ni katika hali ambayo muungano vamizi wa Saudia jana pekee ulishambulia mara 25 wilaya ya Sirwah mkoani Maarib ambapo vikosi vya ulinzi vya jeshi la Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen vimekuwa vikisonga mbele.
Wakati huo huo, jeshi na makundi ya kujitolea ya wananchi wa Yemen pia yameendeleza mashambulizi dhidi ya Saudi Arabia. Brigedia Jenerali Yahya Saree juzi usiku alithibitisha katika ukurasa wake wa twitter kutekelezwa shambulio hilo la kombora katika kituo cha anga cha Mfalme Khalid cha Saudia na kuandika: "Kikosi cha makombora kimevurumisha kombora la balistiki ambalo bado halijazinduliwa kuelekea katika eneo la Khamis Mushait katika kituo cha anga cha Mfalme Khalid". Kombora hilo limelenga kwa makini shabaha iliyokusudiwa." Akijibu kwa nini vikosi vya Yemen vimetekeleza oparesheni hiyo juzi usiku, Brigedia Jenerali Yahya Saree amesema: "Oparesheni hiyo imetekelezwa katika kituo cha Saudia ili kujibu kuendelea mashambulizi ya anga na nchi kavu na nchi vamizi na kuendelea kuzingirwa nchi yetu ya Yemen."
Hata kama matukio haya tajwa yamekaririwa mara kadhaa katika vita vya miaka sita huko Yemen, lakini sasa kuna malengo maalumu yaliyo nyuma ya matukio hayo. Serikali ya Marekani chini ya uongozi wa Rais Joe Biden imetaka kukomeshwa vita dhidi ya Yemen na imesitisha pia uungaji mkono wake kwa muungano vamizi wa Saudia. Serikali ya Saudi Arabia inaendeleza mashambulizi huko Yemen ili kutuma ujumbe huu kwamba haiko tayari kukubali kushindwa. Katika upande mwingine, jeshi na makundi ya kujitolea ya wananchi wa Yemen pia yanaendeleza mashambulizi dhidi ya Aal Saud na kutahadharisha kuwa kuendelea vita huko Yemen hakutakuwa kwa manufaa ya Riyadh na ni vyema utawala huo uuunge mkono na kukaribisha pendekezo lolote la kukomesha uvamizi huko Yemen.
Nukta nyingine muhimu ni hii kuwa, maamuzi ya serikali ya Biden kwa ajili ya kukomesha vita huko Yemen hayatokani na hisia za kibinadamu bali zaidi ya yote yanatokana na kuwa, vita hivyo hadi sasa havijakuwa na manufaa yoyote; bali kuendelea kwake kutapekea tu kuharibiwa zaidi miundombinu ya Yemen na kupunguza pia uzito wa kushindwa Marekani katika vita hivyo. Marekani imekuwa ikiunga mkono muungano vamizi wa Saudia katika vita hivyo. Kwa hiyo Biden anajaribu kutumia vita hivyo kama fursa ya kusafisha taswira ya Marekani duniani; na ataweza kutimiza lengo hilo iwapo atafanikiwa kukomesha vita hivyo. Pamoja na hayo, inapasa kusubiri na kuona je, Joe Biden na serikali yake wataweza kweli kubadili siasa zao za porojo na kuwa siasa za vitendo au la?