Yemen: Kujibu jinai tunazofanyiwa na wavamizi ni haki yetu ya kisheria
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i66876-yemen_kujibu_jinai_tunazofanyiwa_na_wavamizi_ni_haki_yetu_ya_kisheria
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen amesisitiza kuwa, nchi yetu sasa hivi imo vitani, inashambuliwa kila uchao, hivyo ni haki ya kawaida kabisa kwa wananchi wa Yemen kujibu mashambulizi wanayofanyiwa.
(last modified 2026-05-20T03:07:53+00:00 )
Feb 15, 2021 04:22 UTC
  • Yemen: Kujibu jinai tunazofanyiwa na wavamizi ni haki yetu ya kisheria

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen amesisitiza kuwa, nchi yetu sasa hivi imo vitani, inashambuliwa kila uchao, hivyo ni haki ya kawaida kabisa kwa wananchi wa Yemen kujibu mashambulizi wanayofanyiwa.

Naibu huyo wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen amesema hayo usiku wa kuamkia leo Jumatatu katika mtandao wa kijamii wa Twitter na kuongeza kuwa, wavamizi wa nchi yetu bila ya shaka hadi sasa wameshapata ujumbe kwamba jeshi la Yemen halina hamu ya kumshambulia mtu wala kundi lolote lakini ni haki yake kujihami.

Aidha ameziambia nchi vamizi zinazoongozwa na Saudi Arabia na waungaji mkono wao kwamba badala ya kujitia pamba masikioni na upofu machoni na kujifanya kutoona wala kusikia jinai wanazofanyiwa wananchi wa Yemen, madola hayo yatekeleze majukumu yao na yaache kulilaumu jeshi la nchi hiyo kila linapojibu jinai wanazofanyiwa wananchi wa Yemen.

Moto ukiwaka ndani ya Saudi Arabia baada ya kushambuliwa na wanamapambano wa Yemen kujibu jinai wanazofanyiwa

 

Vile vile ameitaka jamii ya kimtaifa kushirikiana na wananchi wa Yemen kuwalazimisha wavamizi wa nchi hiyo kukomesha vita na kuacha kulizingira kila upande taifa hilo la Kiarabu.

Katika upande mwingine, Brigedia Jeneli Yahya Sarii, msemaji wa vikosi vya ulinzi vya Yemen jana Jumapili alitangaza habari ya kushambuliwa uwanja wa ndege wa Abha wa Saudi Arabia na kusema kuwa, maeneo yaliyokusudiwa ndani ya uwanja huo yamelengwa kwa ustadi mkubwa na vikosi vya Yemen ikiwa ni majibu ya jinai zinazofanywa na Saudia dhidi ya wananchi wa Yemen.