Ansarullah: Wito wa Biden wa kusitishwa vita Yemen si wa kweli
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i66984-ansarullah_wito_wa_biden_wa_kusitishwa_vita_yemen_si_wa_kweli
Mjumbe wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen amejibu uvumi unaosambazwa kwamba Marekani inafanya juhudi za kusimamisha mashambulizi dhidi ya Yemen akisema serikali ya Washington ndiyo kinara na kamanda wa mashambulizi yanayofanywa dhidi ya Yemen na sababu kuu ya masaibu ya taifa la nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Feb 18, 2021 06:35 UTC
  • Muhammad Ali al Houthi
    Muhammad Ali al Houthi

Mjumbe wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen amejibu uvumi unaosambazwa kwamba Marekani inafanya juhudi za kusimamisha mashambulizi dhidi ya Yemen akisema serikali ya Washington ndiyo kinara na kamanda wa mashambulizi yanayofanywa dhidi ya Yemen na sababu kuu ya masaibu ya taifa la nchi hiyo.

Muhammad Ali al Houthi amesema kuwa Saudi Arabia na Imarati haziwezi kufanya lolote bila ya ruhusa au maagizo ya moja kwa moja ya Marekani.

Mjumbe huyo wa ngazi za juu wa harakati ya Ansarullah amesema kuwa, Marekani haitaki kuwepo amani na suluhusu nchini Yemen kwa sababu ndiyo inayoongoza mashambulizi na uchokozi dhidi ya nchi hiyo, na kwa maneno mengine tunaweza kusema kuwa, Washington ndiye msababishaji wa maafa yanayolipata taifa la Yemen; hivyo wito wa Joe Biden wa kusitishwa vita si wa kweli. 

Ali al Houthi amesema kuwa, watu wa Yemen wanaelewa vyema kwamba Marekani, Uingereza, Ufaransa, Saudi Arabia, Imarati na nchi za Kiarabu waitifaki katika muungano wa vita dhidi ya taifa la Yemen ndiyo wanaofanya mashambulizi na kutuma silaha za kuua raia wa nchi hiyo. 

Uharibifu wa mashambulizi ya Saudia na washirika wake dhidi ya Yemen

Majuzi Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani na mjumbe wa nchi hiyo katika masuala ya Yemen, Timothy Lenderking alisema kuwa njia ya kisiasa ndiyo chaguo pekee la utatuzi wa mgogoro wa Yyemen na kwamba sasa umewadia wakati wa kukomesha mapigano katika nchi hiyo. 

Mwaka 2015 Saudi Arabia ikisaidiwa na Marekani, Israel, Imarati na nchi nyingine kadhaa zilianzisha mashambulizi makubwa dhidi ya taifa la Yemen na kuizingira nchi hiyo kutokea pande zote za nchi kavu, baharini na angani. Maelfu ya Wayemeni wasio na hatia wameuawa katika mashambulizi hayo na mamilioni ya wengine wamelazimika kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi hiyo.