Oxfam yatahadharisha juu ya siasa za Uingereza kuhusu Yemen
Shirika la misaada ya kibinadamu la Oxfam limekosoa uamuzi wa serikali ya Uingereza wa kupunguza misaada yake ya kibinadamu kwa raia wa Yemen huku ikizidisha misaada yake ya kijeshi kwa utawala wa Saudi Arabia unaoendela kuwaua kinyama raia hao wasio na hatia.
Oxfam umeutaja uamuzi huo kuwa mfano wa wazi wa mgongano uliopo katika siasa za serikali ya London na kuongeza kuwa hiyo ni ishara ya wazi ya viongozi wa serikali hiyo kuwa na moyo wa kinyama.
Oxfam ni moja ya mashirika kumi ya misaada ya kibinadamu ambayo hivi karibuni yalimwandikia barua waziri mkuu wa Uingereza yakikosoa uamuzi wa serikali yake wa kupunguza misaada ya kibinadamu kwa raia wa Yemen.
Serikali ya Waziri Mkuu Boris Jonson ambayo ni mshiriki mkubwa katika mauaji yanayotekelezwa dhidi ya watu wa Yemen, kwa kuiuzia Saudia silaha za mauaji, katika bajeti yake ya mwaka huu imeamua kupunguza msaada wa kibinadamu kwa Yemen kutoka pauni milioni 160 hadi pauni milioni 87.
Nyaraka za kuaminika pia zinaonyesha kuwa serikali ya London imeazimia kupunguza pakubwa msaada wake wa kibinadamu kwa Syria mwaka huu kutoka pauni milioni 137 hadi milioni 45 pekee.
Hii ni katika hali ambayo ripoti zilizopo zinaonyesha kwamba nchi hiyo haijapunguza popote msaada wake wa silaha kwa utawala wa Saudia ambao unaongoza hujuma ya kikatili ya kijeshi dhidi ya watu wa Yemen. Wanaharakati wa haki za binadamu wamethibitisha kwamba Uingereza jivi karibuni imeiuzia Saudia silaha zenye thamani ya pauni bilioni 1.4 baada ya kuondolewa marufuku ya mauzo hayo ya silaha kwa nchi hiyo ya Kiarabu.
Tokea Yemen ivamiwe na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia mwaka 2015 hadi sasa, Uingereza imeiuzia nchi hiyo ya Kiarabu inaoongozwa kifalme silaha zenye thamani ya karibu pauni bilioni 5 na pia kuipia msaada mkubwa wa mafunzo ya kijeshi.