Makundi ya Muqawama Palestina yauonya utawala wa Kizayuni wa Israel
Makundi ya muqawama na kupigania ukombozi wa Palestina yametoa onyo kali kwa utawala wa Kizayuni wa Israel kuhusu kuchukua hatua zozote za kuwakandamiza vijana Wapalestina katika mji wa Quds (Jerusalem) unaokaliwa kwa mabavu.
Televisheni ya Al Alam imetangaza kuwa makundi ya muqawama yametoa taarifa Jumanne Wapalestina wasiondoke katika Msikiti wa Al Aqsa baada ya Sala na Itikafu ili wakabiliane na walowezi wa Kizayuni ambao wanataka kuuhujumu msikiti huo.
Taarifa hiyo imesema kuwa, Mji wa Quds ni wa Kiislamu na Kiarabu na utabakia hivyo. Aidha taarifa hiyo imesema kuwa mji wa Quds utabakia kuwa mji mkuu daima wa taifa la Palestina na kwamba Wazayuni maghasibu hawana nafasi yoyote katika mji huo na ardhi zote za Palestina.
Makundi ya kupigania ukombozi wa Palestina yamesisitiza kuwa, mapambano yao na utawala ghasibu wa Israel mjini Quds yanahusu utambulisho na uwepo. Aidha taarifa hiyo imesema ule 'Muamala wa Karne' wa Trump, kutekwa ardhi za Palestina na baadhi ya nchi za Kiarabu kuanzisha uhusiano na utawala bandia wa Israel yote hayo yako katika mkondo wa kuporomoka na ushindi hatimaye utakuwa ni wa umma wa Kiislamu.

Makundi hayo ya muqawama pia yamewataka wakazi wa Ukingo wa Magharibi, Quds, na ardhi zote zinazokaliwa kwa mabavu waende kuwasaidia Wapalestina katika eneo la Sheikh Jarrah mashariki mwa mji wa Quds.
Hivi karibuni mahakama moja ya utawala wa Kizayuni wa Israel ilitaoa hukumu ya kuzitaka familia kadhaa za Wapalestina katika eneo la Sheikh Jarrah kuondoka katika nyumba zao ambazo sasa zitachukuliwa na Walowezi wa Kizayuni. Wapalestina wameapa kutoondoka katika nyumba hizo zao za jadi.